Misri kuandaa AFCON 2019, waiangusha Afrika Kusini

Muktasari:

 

  • Mataifa kadhaa yalijitokeza ambapo upinzani mkubwa ulikuwepo kati ya Afrika Kusini na Misri, ambapo wengi walikuwa wakiipigia chapuo  Afrika Kusini.

Dakar, Senegal. Hatimaye Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limeithibisha Misri kuwa ndiye mwenyeji wa michuano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Egypt inachukua nafasi ya Cameroon.

Awali Cameroon, ilikuwa imepata nafasi ya kuandaa makala hayo ya 32, lakini wakavuliwa kutokana na kushindwa kukamilisha maandalizi ya viwanja na miundombinu muhimu yatakayotumiwa na mataifa zaidi ya 24, washiriki wa michuano hiyo.

Mara baada ya Cameroon kupokonywa haki ya kuandaa michuano hiyo, mataifa kadhaa yalijitokeza ambapo upinzani mkubwa ulikuwepo kati ya Afrika Kusini na Misri, ambapo wengi walikuwa wakiipigia  Afrika Kusini, ambao walikuwa wenyeji wa Kombe la Dunia 2010, kuandaa fainali za mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya mashindano ya CAF, iliyokaa leo mjini Dakar Senegal,Misri  ilikidhi vigezo vyote na hivyo kukabidhiwa jukumu la kuandaa kipute hicho, kinachotarajiwa kutimua vumbi kati ya Juni 15 na Julai 13, kwa maana kwamba Misri ina miezi sita tu ya kukamilisha maandalizi.

Aidha, licha ya kupokonywa nafasi ya kuandaa makala ya mwaka huu, Cameroon, itakuwa mwenyeji wa makala ya 33, itakayofanyika mwaka 2021. Kutoka Afrika Mashariki, Kenya na Uganda, tayari zimeshakata tiketi ya kwenda AFCON 2019.