Messi ataja nne zinazomtisha Ulaya

Muktasari:

Miaka mitatu ya kuishia kwenye robo fainali waliivunja msimu uliopita wakati walipowasukuma nje Manchester United na kutinga nusu fainali ambako walikutana na Liverpool. Mechi ya kwanza walishinda 3-0 uwanjani Nou Camp, kabla ya kwenda kufanyiwa maajabu Anfield, walipokwenda kuchapwa 4-0 na kusukumwa nje.

BARCELONA, HISPANIA . SUPASTAA, Lionel Messi amedai kwamba Liverpool, Real Madrid, Juventus na Paris Saint-Germain ndizo timu zitakazokuwa tishio kwa Barcelona kwenye mpango wao wa kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Chama hilo la Messi litakabiliana na Napoli kwenye hatua ya 16 bora na hakika kwa sasa presha imekuwa kubwa kwenye kuifukuzia fainali yao ya kwanza kwenye michuano hiyo ya Ulaya tangu 2015.
Miaka mitatu ya kuishia kwenye robo fainali waliivunja msimu uliopita wakati walipowasukuma nje Manchester United na kutinga nusu fainali ambako walikutana na Liverpool. Mechi ya kwanza walishinda 3-0 uwanjani Nou Camp, kabla ya kwenda kufanyiwa maajabu Anfield, walipokwenda kuchapwa 4-0 na kusukumwa nje.
Messi sasa anataka kubeba taji hilo ili kuongeza medali yake ya tano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, amesema kuna ugumu mbele yao, akizitaja klabu nne ambazo zinawafanya wao Barcelona wakose usingizi kwenye mipango yao ya kubeba ubingwa.
Messi alisema: “Timu zinasumbua na ni ngumu. Paris wameenda kucheza na Dortmund na wamepoteza, Liverpool walienda kwa Atletico nako pia wamepoteza. Ila nadhani Liverpool, Juventus, Paris na Madrid ndizo timu ngumu msimu huu.”
Licha ya kuwapa nafasi vijana wa Jurgen Klopp mwaka huu, Messi anaamini pia Atletico ina uwezo mkubwa wa kulinda ushindi wao wa bao 1-0 wakati watakapokwenda Anfield – kitu ambacho Barca walishindwa.