JICHO LA MWEWE: Mbwana Samatta anatatua tatizo kubwa la msingi

MUDA wowote kuanzia sasa Mbwana Ally Samatta atatangazwa kuwa mchezaji mpya wa Klabu ya Aston Villa. Mabingwa mara saba wa Ligi Kuu ya England. Moja kati ya timu kongwe na zenye historia nzuri katika soka la England. Klabu inayotoka katika jiji la pili kwa ukubwa England, Birmingham.

Anapotangazwa kuwa mchezaji wa Aston Villa akitokea Klabu ya Genk ya Ubelgiji, huku akiwa amezaliwa Mbagala jijini Dar es salaam, Samatta anavunja mzizi wa fitina uliojengeka kwa miaka mingi iliyopita. Anawaaminisha Wazungu kwamba kuna mchezaji wa Kitanzania anaweza kucheza Ligi Kuu ya England.

Hapa anatatua tatizo la msingi sana. Kabla yake hakuna mchezaji wa Kitanzania aliyewahi kucheza katika ligi tano kubwa za Ulaya ambazo ni England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa. Samatta anakuwa mchezaji wa kwanza. Baada ya hapo Wazungu ukiwapelekea mchezaji wa Kitanzania mezani wataamini kwamba “inawezekana, anaweza”. Kabla ya hapo hawakuwa na sababu ya msingi ya kuamini.

Kama historia ya Samatta ingeonyesha amezaliwa Copenhagen, Demark au Mallorca pale Hispania, Wazungu wasingepata wakati mkubwa wa kuamini. Wangehisi kwamba ameweza kwa sababu amepitia katika mikono yao tangu katika kitanda cha hospitali. Lakini sasa wanaweza kuamini kwa sababu Mbwana amezaliwa Tanzania, amekulia Tanzania, akaenda kucheza soka la kulipwa DR Congo kisha akaibukia Ubelgiji kabla ya kutua England. Kuanzia sasa wataamini kwamba kuna mchezaji wa Kitanzania anaweza kupitia njia hizo na kufika ligi kubwa za Ulaya.

Wachezaji wengi wa Kitanzania wamekuwa wakipata wakati mgumu wakati wanapofanya majaribio huku wakishindana na wachezaji kutoka Afrika Kaskazini au Afrika Magharibi. Kocha au tajiri wa timu anaamua kumchukua mchezaji kutoka Nigeria kwa sababu anaamini anatoka katika taifa la soka na lazima atakuwa anajua mpira zaidi kuliko yule anayetoka Tanzania.

Hapa ndipo Samatta anapomaliza tatizo la msingi. Akifunga mabao zaidi ya 15 ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu ya England atazidi kuwasaidia vijana walio nyuma yake ambao wanataka kucheza soka la kulipwa barani Ulaya. Ligi Kuu ya England inatazamwa na mashabiki zaidi ya bilioni moja duniani kote kwa mwaka. Samatta atatazamwa zaidi katika mechi kibao za nyumbani na ugenini dhidi ya Arsenal, Manchester United, Manchester City, Liverpool, Chelsea, Tottenham na wengineo. Lakini pia atatazamwa katika michuano mingine kama Carabao na FA.

Kenya walitatua tatizo hili kuanzia pale McDonald Mariga alipocheza klabu kubwa kama Inter Milan. Lakini mdogo wake, Victor Wanyama akatatua zaidi wakati alipotua Southampton na kuwa mchezaji wa kwanza wa Kenya kucheza Ligi Kuu ya England. Aliposogea Tottenham ilikuwa faida kubwa zaidi. Leo Wazungu wanaamini Mkenya anaweza kucheza mpira katika kiwango cha juu. Sio tu Mkenya aliyezaliwa Ulaya kama Divork Origi, lakini wanajua Mkenya aliyezaliwa Nairobi kama Wanyama anaweza kucheza katika kiwango cha juu zaidi. Unapoona mchezaji wa kimataifa wa Zimbabwe kama Marvelous Nakamba anacheza Aston Villa ni kwa sababu pia kwa miaka mingi Wazungu wanaamini mchezaji anaweza kutoka katika nchi ya Zimbabwe.

Historia ilishawekwa pale na staa wa zamani wa Zimbabwe, Peter Ndlovu ambaye alikuwa staa wa kwanza wa Afrika kucheza Ligi Kuu ya England ilipoanzishwa mwaka 1992.

Kwa mchezaji wa Ligi Kuu ya Tanzania kucheza Ligi Kuu ya England si mara ya kwanza. Nonda Shaban Papii aliwahi kutoka Yanga akasafiri huku na kule akaibukia Blackburn Rovers. Hata hivyo Nonda alikuwa Mcongo. Hakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Congo kucheza ligi kubwa Ulaya, kwa hiyo lilikuwa jambo la kawaida tu kwa Wazungu kuamini.

Samatta anaandika historia nzito katika taifa letu. Analeta mabadiliko makubwa ya kifikra kwa namna ambavyo Wazungu wamekuwa wakitutazama kwa miaka nenda rudi. Kilichobaki kwa sasa ni kwa vijana kujituma kwa sababu njia imefunguliwa.

Samatta hatadumu milele. Ana miaka kama mitano hivi ya kucheza soka katika kiwango cha juu. Alichofanya ni kufungua njia tu kwa wengineo. Lakini pia kwa mtazamo mwingine ni kwamba hata wachezaji wa Kitanzania nao wataamini kwamba inawezekana.

Kwa mfano, kwa Kelvin John mambo mawili yametokea. Klabu ya Genk imeona inawezekana kwa mchezaji wa Kitanzania kutamba Ulaya. Na sasa imemuweka Kelvin katika mikono yao. Lakini hapo hapo na Kelvin ameona inawezekana na ndio maana amesafiri mpaka Genk kwa ajili ya kujiunga na klabu hiyo japo umri haumruhusu kwa sasa na amelazimika kuwekwa England kwa muda.

Kama kila mmoja akiona inawezekana. Kuanzia upande wao hadi wetu, basi maisha yatakuwa rahisi zaidi kwa wachezaji wetu na tutajitokeza vema katika ramani ya soka. Muda si mrefu tutashindana katika majaribio na wenzetu kwa sababu ya uwezo wetu na hatuwezi kushindwa kwa sababu ya Utanzania wetu kama ilivyokuwa awali.