Matajiri wamaliza kazi

HALI ndani ya klabu ya Yanga jana ilichafuka kwa muda baada ya nyota wa timu hiyo kufanya mgomo baridi wa kususia mazoezi, jambo lililomshangaza Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera na kuchimba mkwara mzito kabla ya matajiri wa klabu hiyo kuingilia kati na kuumaliza mgomo huo kiaina.

Nyota wa Yanga waliamua kugomea mazoezi yaliyokuwa yafanyike kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam wakishinikiza kulipwa malimbikizo ya fedha zao wanazoidai klabu hiyo, jambo lililomfanya Zahera acharuke na kuchimba mkwara wa kuwatimua wasiofika mazoezini leo.

Hata hivyo, mara baada ya mabosi wa Yanga kuona hali inayoendelea, fasta waliamua kuzungumza na Kocha Zahera, kisha mchezaji mmoja mmoja kupigiwa simu ili kulainishwa na leo wameahidi kufika kuendelea na mazoezi yao kama kawaida, lakini ni baada ya kuhakikishiwa mambo.

Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa na baadhi ya nyota wa klabu hiyo kwamba wamegomea mazoezi kushinikiza kulipwa chao, hasa baada ya kushtushwa na taarifa kuwa michango inayoendelea kukusanywa ni maalum kwa usajili msimu ujao.

Zahera alisema wachezaji wote waliogomea mazoezi jana endapo watashindwa kuhudhuria tena na leo basi wabaki tu majumbani hadi mwisho wa msimu.

Hata hivyo, mkwara huo hautawagusa, beki Kelvin Yondani na Papy Kabamba Tshishimbi aliodai ana taarifa zao za kushindwa kuhudhuria mazoezini jana.

Alisema ameshtushwa na walichofanya wachezaji hao kwani katika maisha yake ya soka hajawahi kuwasimamia wachezaji kama anavyofanya Yanga, huku wakifanya mgomo huo bila hata kumtaarifu.

“Hata wachezaji sidhani kama wapata mtu kama mimi, nimekuwa nikiwasaidia mambo mengi ndani na nje ya uwanja pamoja na maisha yao tangu nimefika hapa, nimesikitishwa na hiki walichokifanya,” alisema Zahera na kuongeza;

“Baada ya kukosekana mazoezini, nimeongea na Hafidh Saleh awaambie kwa yeyote atakayekosa mazoezi ya kesho (leo) asirudi tena, haiwezekani wachezaji wakaanza kugomea mazoezi mwezi mmoja kabla ya kumaliza ligi.”

Zahera alisema ishu ya malimbikizo ya mishahara haijaanza sasa, ipo tangu zamani na kila mmoja anatambua wanadai ila anashangaa kwanini waligoma jana na kuhoji kuwa wachezaji wanatakiwa kuulizwa mishahara yao ya mwisho wamepewa lini.

ISHU MICHANGO

Inaelezwa kilichowavuruga nyota hao wa Yanga ni zoezi la changia Yanga linaloendelea chini ya Mwenyekiti Anthony Mavunde lililozinduliwa Dodoma likiwa na lengo la kukusanya Sh1.5 bilioni kwa ajili ya kuboresha kikosi chao msimu ujao.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti jana asubuhi wachezaji hao wa Yanga walisema wanaumizwa na uamuzi unaofanywa na kampeni hiyo kulenga zaidi usajili wa msimu ujao wakati wao wanateseka hawana malipo ya mishahara.

MATAJIRI WAUZIMA

Hata hivyo, jioni ya jana baada ya mabosi wa Yanga kufuatilia ishu ya mgomo huo, waliitana fasta na matajiri wanaoipiga tafu timu hiyo na kujadiliana kwa kina hasa baada ya kusikia kilichowafanya nyota hao kugoma na kuweka mambo sawa wakiwaomba nyota wote wafike mazoezini leo ili wamalizane.

Hatua ya viongozi kuwaita nyota hao mazoezini leo ili kumaliziana nao imetokana na ukweli kwa sasa Yanga haipo kambini na wachezaji wanatoka makwao, kitu kilichowakwamisha mabosi na matajiri wao kumalizana jioni ya jana na kuamua kuwaita wakieleza kila kitu kitakuwa poa.

“Tumepigiwa simu jioni hii (jana) kwamba kila kitu kitakuwa freshi kwani ni ishu ndogo na tumeambiwa wote tufike mazoezini saa 2 ili kabla ya kuanza tuzungumze kisha mengine yaendelee, nasi hatuoni tatizo, kwani lengo ni kutaka kujua hatma yetu itakuwaje klabuni,” alisema mmoja ya wachezaji wa Yanga aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Kabla ya wachezaji hao kufichua hatua na mabosi wao kutaka suluhu, Mwanaspoti lilimsaka Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya Yanga, Lucas Mashauri ili kujua kinachoendelea juu ya mgomo huo baridi ambao umekuja ligi ikiwa inaelekea ukingoni na kudai hakufahamu lolote.

“Ndiyo kwanza wewe unanifahamisha, ngoja nifuatilie,” Mashauri alijibu kwa kifupi na kukata simu, ingawa Mwanaspoti linafahamu mapema asubuhi ya jana alienda mazoezini saa 4:30 asubuhi na kukuta wachezaji wameshasepa na kuwaacha watu wa Benchi la Ufundi wakijadiliana na kumjulisha.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omar Kaaya aliposakwa ili kufafanua juu ya jambo hilo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.