HISIA ZANGU : Mastaa wanapishana Airport kwa sababu ya mbwana Samatta

Muktasari:

  • Mastaa wa Kibongo hawa akina Ambokile hawajataka hata kugusa Simba na Yanga. Fursa zimetokea na wamechangamkia. Zamani wangependa kwanza waende kucheza timu za Kariakoo ambazo kaka zao kina Shadrack Nsajigwa wamepita.

ELIUD Ambokile wa Mbeya City amekwenda Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa, Shiza Kichuya amekwenda Misri. Mastaa wetu wanapishana Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pale Kipawa. Limeanza kuwa jambo la kawaida.

Muda mrefu sana nilijua tulihitaji shujaa mmoja kwa ajili ya kunyanyua wengine. Sio lazima awalipie nauli. Sio lazima awapeleke awalipo. Shujaa wa kuonyesha inawezekana. Na sasa baada ya Tanzania kutoa Mfungaji Bora katika Ligi Kuu ya Ubelgiji nadhani wenzake wanaona inawezekana.

Wanaona inawezekana kuishi nje, kuthaminiwa kama unavyothaminiwa nyumbani, kupata pesa, kuwa staa na kuishi maisha mazuri. Mbwana Samatta amesaidia katika hili. Naanza kuona vijana hawaogopi tena kutoka.

Alipoondoka Nonda Shaaban kwenda Afrika Kusini na kisha kutamba Ulaya, wachezaji wengi wa zama zake waliamini Nonda alikuwa amefanikiwa kwa sababu sio Mtanzania. Ilionekana Utanzania ni tatizo.

Kabla ya hapo tatizo kubwa halikuwa mawakala wala klabu. Tatizo kubwa lilianzia katika mioyo ya wachezaji wenyewe. Hawakujiamini na hawakutaka kutoka. Viongozi wa klabu walikuwa wanatumia fursa tu ya ujinga wa wachezaji kuwabakiza, lakini ukweli ni kwamba moyo wa mwanadamu ukiamua jambo ni ngumu kuzuia.

Mastaa wa Kibongo hawa akina Ambokile hawajataka hata kugusa Simba na Yanga. Fursa zimetokea na wamechangamkia. Zamani wangependa kwanza waende kucheza timu za Kariakoo ambazo kaka zao kina Shadrack Nsajigwa wamepita.

Mastaa wetu sasa wanaamini inawezekana. Tulihitaji mtu wa namna hiyo na tumempata kupitia Samatta. Halafu Thomas Ulimwengu. Halafu Simon Msuva ambaye kila siku tunamuona anatupia mabao kule Morocco.

Kitu pekee ambacho Samatta hajawatia moto wachezaji wetu ni aina yake ya maisha. Bahati nzuri au mbaya Samatta ni mpole na mkimya. Maisha yake mengi binafsi ameyaweka siri. Kama angeamua kuishi maisha ambayo Denis Oliech aliishi Kenya katika enzi za ustaa wake nadhani wachezaji wengi wangezidi kukimbia nchini.

Watu wengi hawafahamu Samatta analipwa kiasi gani. Kumbuka analipwa kwa Euro. Watu wengi hatufahamu Samatta anamiliki nini. Bahati nzuri pia sio mtu wa kuja Dar es salaam akazurura na magari ya bei mbaya. Najua anayo, lakini anajifungia katika vioo.

Wazazi wengi wangepeleka vijana wao katika soka kama Samatta angeweka wazi utajiri wake na kiasi anacholipwa kwa wiki pale Ulaya. Bahati mbaya maisha ya aina hii ameyaweka sirini na hakuna ambacho tunaweza kufanya.

Kabla hata hajagusa Genk, Samatta angeweza kuwashawishi vijana wengi kutamba nje ya Tanzania kama angewaambia kiasi gani alikuwa analipwa wakati anakipiga na TP Mazembe. Alikuwa anapata kiasi kikubwa cha pesa ambacho kingeweza kuwatia wazimu wachezaji wetu wengi, lakini aliamua kuwa kimya.

Pale Nigeria vijana wengi huchomoka kwa sababu utajiri wa wachezaji wao upo wazi. Kina Jay Jay Okocha wakati wanalipwa mamilioni ya pesa kule Ulaya ungeweza kuona magari yao ya bei mbaya pamoja na mbwembwe nyingi.

Samatta hayupo hivyo. Matokeo yake wachezaji wengi wanamuangalia zaidi kwa mafanikio yake uwanjani, lakini sio mali zake.

Kuna wachezaji wengi nawafahamu ambao kama wangekuwa Samatta tungejua thamani ya saa anayovaa au thamani ya miwani anayovaa. Bahati mbaya kwa Samatta ni hawezi kuishi maisha hayo. Ninachofahamu ni kwamba kipesa Samatta anaishi maisha ambayo ni ndoto ya wengi.

Vyovyote ilivyo hatuwezi kuwa na timu ya taifa iliyo imara kama wachezaji wetu hawatachomoka na kwenda kutengeneza majina nje ya nchi. Tayari tumeanza kupata msaada pale Taifa Stars kupitia kwa kina Samatta na Msuva ambao wameleta vitu tofauti.

Tatizo pekee ambalo linaanza kutukabili kwa sasa ni ukweli wachezaji wengi ambao wanapata fursa hizi ni wale wanaocheza katika nafasi ya ushambuliaji. Kiungo anayecheza nje ni Himid Mao Mkami tu wakati beki ni Abdi Banda na Hassan Kessy tu. Hawa Samatta, Msuva, Ulimwengu, Rashid Mandawa, Ambokile, Kichuya na hata kina Farid Mussa na Shaaban Idd Chilunda, wote ni washambuliaji.

Hatuwezi kwenda hivi. Tunahitaji makipa wanaocheza soka la kulipwa katika Ligi za kishindani. Tunahitaji mabeki wengi wanaocheza soka la kulipwa katika nje ya mipaka yetu. Tutapata uwiano mzuri wa kimchezo kama wachezaji wa nafasi nyingine wakiitwa kutoka katika klabu za nje.

Ligi yetu imeendelea kututhibitishia haiwezi kutupa Taifa Stars kwa sababu hata hizi timu kubwa kwa sasa zinatawaliwa na wachezaji wa kigeni. Pale Simba katika pambano la Jumamosi usiku dhidi ya Al Ahly pale Misri walianza wachezaji nane wa kigeni. Ni wazi wachezaji wa nyumbani hawana nafasi.

Namna pekee ya kuitengeneza Taifa Stars iliyo imara kwa njia ya mkato ni kwa namna hii ambayo kina Ambokile wanaunga mkono juhudi za kina Samatta.

Na hata hawa watoto wa Serengeti Boys nao tuwafungulie zaidi milango. Watatupeleka mbali. Kwa sasa wanaamini kwa sababu wanamuona Samatta.