Mastaa waitumie leo kuikumbuka kesho yao

TASNIA ya soka kwa wiki moja na ushei imekuwa na majanga ya kupoteza nyota wake wakiwamo wa zama hizo na wale waliopita. Said Mrisho ‘Zico wa Kilosa’, Barnabas Sekelo na juzi tu Said Mtupa wote wametangulia mbele ya haki.

Wawili, Sekelo na Mtupa wamekumbwa na mauti kutokana na ajali ya bodaboda kila mmoja kwa wakati wake, huku Zico akifariki kutokana na kuugua. Inasikitisha, hata kama ni kweli kila nafsi ni lazima ionje mauti kwani sisi ni wa Allah SW na kwake lazima tutarejea tu!

Hata hivyo kwenye mazishi wa Zico, Mwenyekiti wa Umoja wa Mavetarani wa Soka nchini (UMSOTA) Paul Lusozi ‘Father’ alizungumza jambo moja linalopaswa kuzingatiwa na kufanyiwa kazi na wachezaji wa sasa kazi kwa mustakabali wa maisha yao ya kesho.

Father Lusozi aliyewahi kucheza Pan Africans na Toto Africans alisema kuna mahali nyota wa zamani walikwama, lakini wachezaji wa sasa hawapaswi kufuata nyayo hizo na badala yake watumie fedha wanazovuna kipindi hiki kujiwekea akiba kwa siku za baadaye.

Hakuna ubishi nyota wa zamani hawakuwa wakivuna fedha za kutosha kama wa kipindi hiki, lakini bado kuna baadhi yao wanaisahau kesho yao kwa kuitumikia leo, hivyo lazima waamke sasa kama hawapendi kuaibika uzeeni kama inavyowatokea waliowatangulia.

Kwa kuwa nyota wa sasa wanavuna fedha kuanzia kwenye sajili zao mpaka malipo ya mishahara na posho, akili zao lazima ziamke na kujiwekea akiba ya kutosha ama kuwekeza kwenye rasilimali ambazo zitakuja kuwasaidia watakapostaafu soka.

Maisha ya soka ni mafupi mno, tofauti na yale ya kawaida, ndio maana waliostaafu bila kuweka mipango sawa wamekujikuta wakiishi kwa dhiki wakitegemea nguvu za rafiki, jamaa na mashabiki wao wanaojitolea kuwasaidia wanapokuwa na matatizo. Haivutii!

Ndio maana nimekazia kauli ya Father Lusozi kuwa, kuna maisha nje ya soka na nyota wa sasa lazima waikumbuke na kuitumikia leo kwa manufaa ya kesho yao ambao ni ndefu na yenye changamoto nyingi hasa wanapokuwa wameshastaafu, kwani akiba huwa haiozi!