Masharti aliyopewa Fundi Simba mazito!

ULE mvutano wa mabosi wa Simba dhidi ya maamuzi kuhusu kiungo, Msudan Sharaf Eldin Shiboub kuongezewa mkataba umemalizika kwa pande zote mbili kufikia mwafaka.

Muafaka ni kwamba kama Shiboub katika mechi kumi zilizosalia akicheza vizuri na kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa katika mchezo wake wa kwanza wa kimashindano wa Ngao ya Hisani dhidi ya Azam FC basi ataongezwa mkataba wa mwaka mmoja.

Mmoja wa viongozi wa juu Simba, ameliambia Mwanaspoti kuwa wamekubaliana kumpa Shiboub mechi hizo kumi za ligi walizobaki nazo na kama atauwasha moto mkataba mpya ataukuta mezani.

“Unajua Shiboub hajatumika ipasavyo katika timu kutokana na ushindani wa namba, lakini kutokuwa na maelewano mazuri na kocha Sven Vandebroeck, nayo ni changamoto na sasa tumekubaliana kumwangalia kwenye mechi hizo,” alisema na kuongeza:

“Jambo lingine ambalo nilikuwa nawaambia tunamuacha Shiboub, ambaye hajatumika tunakwenda kumpata kiungo wa aina yake wapi?

“Nikutoe tu wasi wasi na kumpa mkataba mwingine, naamini Shiboub atacheza katika kiwango cha juu, hajachuja,” alisema kiongozi huyo na kuongeza watampa mkataba wa mwaka kama ilivyo kwa beki Paschal Wawa.

Mechi kumi ambazo Simba wamebaki nazo kwenye ligi ni dhidi ya Ruvu Shooting, Mwadui, Mbeya City, Tanzania Prison, Ndanda, Namungo, Mbao, Alliance, Coastal Union na Polisi Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema malengo ya timu hiyo kwa sasa ni kumaliza ligi vizuri kwa maana ya kuchukua ubingwa huko pamoja na Kombe la FA.

Senzo alisema baada ya hapo ndio wataanza mipango na mikakati ya usajili wa maana kulingana na mapungufu ya kikosi chao kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.

“Hatutakuwa na usajili mkubwa hivyo, kwa maana ya wachezaji wengi kama misimu kadhaa iliyopita bali tutasajili wachache kutokana na mapungufu ambayo tumeyaona msimu huu,” alisema na kuongeza:

“Ili timu iweze kufanikiwa au yenye mafanikio lazima ikae na wachezaji wake muhimu kwa muda mrefu kwa maana hiyo, hilo ndio tunataka kulifanya msimu huu kwa kuwaongezea mikataba mipya wachezaji wetu ambao, wanamaliza na bado huduma yao inahitajika,” alisema Senzo.