Mashabiki wekeni ushabiki kando mjitokeze kuiunga mkono Simba

Muktasari:

Simba itaikaribisha AS Vita ya DR Congo katika mechi kali ya kufa au kupona itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

KESHO Jumamosi usiku, wawakulishi Pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki, Simba itatupa karata yake ya mwisho katika Kundi D ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itaikaribisha AS Vita ya DR Congo katika mechi kali ya kufa au kupona itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Simba inahitajika kushinda mchezo huo ili isonge mbele kuingia robo fainali ya michuano hiyo. Haijawahi kutokea kwa klabu za Tanzania kucheza hatua hiyo tangu mfumo wa michuano hiyo ulipobadilishwa mwaka 1997.

Hivyo hii ni nafasi adimu kwa Simba na Tanzania kwa jumla. Kila mdau wa soka bila kujali itikadi yake ni wazi angependa kuona historia ikiandikwa kwa Simba ikitinga robo fainali.

Kuingia kwa Simba maana yake ni kwamba wanabakiza hatua chache kabla ya kutinga nusu fainali na kutoa fursa ya Tanzania kuingiza timu NNE katika michuano ya CAF.

Lakini hili la Simba kupenya haliwezi kutokea kama mashabiki hawataungana pamoja kuisapoti Simba kwa kishindo kesho...Ile utamaduni na kasumba ya kuendekeza Usimba na Uyanga unapaswa usahauliwe kabisa.

Kesho ni nafasi ya Tanzania kuweka rekodi, kwa nini tusiungane kuhakikisha rekodi hiyo inatimia na Taifa letu linafaidika kisoka.

Wakati mashabiki wakiungana pamoja na kuishangilia kwa fujo Simba kama njia ya kuwapa nguvu vijana kupata matokeo, wachezaji wa Wekundu wa Msimbazi nao wajitume, wajitoe ili kufanikisha lengo la kuwaona Wawakilishi wa Tanzania wakiipata fursa hiyo.

Nyota wa Simba ndio walioshikilia hatma ya timu yao kusongabele au la! Hivyo lazima wapambane kweli kweli kisha mchezaji wa 12, yaani mashabiki nao watie nguvu kuweka mambo sawa na rekodi iandikishwe....inawezekana kabisa.

Mwanaspoti linawahimiza wachezaji watumize wajibu wao uwanjani na mashabiki nao wafanye yao bila kujali ushabiki ili Simba ikifuzu iwe furaha ya wote.

Simba ina kila sababu ya kukata tiketi ya robo fainali, kwani inacheza nyumbani, pia rekodi zinaibeba nyumbani, kwa nini isikomae?!

Mashabiki na wadau wa soka ni wazi wanasubiri kwa hamu mtanange huo na watajitokeza kwa wingi kuiuynga mkono klabu hii pekee katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki ikitinga hatua hii muhimu kwa taifa letu.

Kutokana na umuhimu wake, dua zinahitajika ikiwamo kuishangilia kwa nguvu Simba ili kuwapa morali ya kufanya vyema.

Simba ina kikosi kipana na mara zote imekuwa ikipata matokeo kwenye uwanja wa nyumbani kwenye mechi za kimataifa.

Tunaamini Jumamosi itakuwa ni mwendelezo tu wa kile Simba walichozoea kukifanya kuhakikisha AS Vita hawatoki Taifa utakaokuwa umejaza mashabiki 6,000.

Hata hivyo ni wakati sasa wa kuachana na kasumba hiyo kwa ajili ya taifa letu. Tubadilike na tujione sisi ni taifa moja inapotokea timu moja inacheza na nyingine ya nje.

Uyanga na Usimba uishie kwenye mechi za Ligi Kuu na michuano mingine ambayo timu hizi kongwe zinashiriki kwani zimekuwa watani wa jadi kwa kipindi kirefu.

Michuano hii haina tofauti na ya timu za taifa kwani hushirikisha mataifa mengi ingawa ni kwa ngazi ya klabu. Lakini hiyo tu inatosha kutufanya sisi Watanzania tuangalie utaifa kwanza na si tu upinzani kwani mwishowe wanaofaidika ni sisi na si nchi nyingine.

Kwa nini tuziachie nchi nyingine ziendelee kutamba kwenye michuano ya ngazi ya klabu ilhali hata nchi yetu inaweza kufanya hivyo? Maendeleo ya soka letu kwa ngazi ya klabu yanaletwa si tu na timu zenyewe, bali na mashabiki pia pale watakapoamua kuungana kwa ajili ya taifa.

Mfano, kwani mashabiki wa Yanga wakiungana na wale wa Simba kwa ajili ya kufanikisha ushindi wao dhidi ya AS Vita ni nini kitatokea zaidi ya Simba kuendelea kuipeperusha Bendera ya Taifa Kimataifa?

Kwani siku ikiwa hivyo kwa Yanga na mashabiki wa Simba wakaipa sapoti kuitoa mfano TP Mazembe itakuwa ni hasara kwa Simba au faida kwa Taifa?

Ndio maana Mwanaspoti tunasisitiza mashabiki waungane bila kuangalia Usimba na Uyanga na wajitokeze kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi saa 1:00 usiku na kuishangilia Simba mwanzo mwisho ili iandike historia kwa taifa letu na kulifanya soka letu lizidi kuimarika katika ukanda huu ambao umekuwa ukibaki nyuma kwa miaka mingi tofauti na kanda nyingine za Afrika.

Tunaamini hilo linawezekana na mashabiki watakuwa kitu kimoja kuipa sapoti Simba kuhakikisha Vita anakaa, kwani siku zote umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.