Mashabiki wauponda msaada wa Diamond

Muktasari:

Hawa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kujaa maji kwenye ini, na matibabu ya tatizo hilo ili kukamilika inahitajika takribani Sh50 milioni ambazo Mwanamuzi Diamond ameahidi kumsaidia.

 

Dar es Salaam. Siku moja baada ya msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz kueleza kuwa anashughulikia matibabu ya Hawa kwenda nchini India, baadhi ya mashabiki wameuponda msaada huo kuwa umechelewa.

Hawa Said maarufu kwa jina la ‘Hawa Nitarejea’ ana zaidi ya mwezi sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa kujaa maji tumboni kulikosababishwa na tatizo la ini.

Kutokana na ugonjwa huo ameshalazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zaidi ya mara nne na kutolewa maji tumboni ambapo kuna wakati alikuwa akitolewa hadi lita nne.

Pamoja na kuugua huko, inaelezwa hakuna wasanii waliojitokeza kumsaidia kama ilivyo kawaida yao mwenzao anapougua, huku shutuma nyingi zikimwangukia Diamond ambaye ndiye mtu aliyemuibua kwenye sanaa.

 

Jana usiku kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Diamond aliandika ‘Niko namshughulikia now kwenda kutibiwa ila sikutaka kutangaza….sitaki watu wachukulie msaada wangu ni kiki…Kwa kuwa maswali  yamekuwa mengi juu yake, imebidi nijibu na matibabu yake sio chini ya milioni 50 na nitadeal nayo tu,”aliandika Diamond hatua iliyopongezwa na wengi.

Kwa upande wake mlezi wa Hawa anayesimamia matibabu yake, Pilli Misanah, ambaye ni mmiliki wa kituo cha kulea waathirika wa dawa za kulevya, amesema maamuzi hayo ya Diamond yalikuja muda mfupi baada ya Hawa kuruhusiwa kutoka Hospitali na kubainika kwamba anatakiwa kwenda nchini India kwa uchunguzi zaidi.

“Ni kweli Diamond tumekuwa tukiwasiliana naye tangu Hawa athibitike kuwa hawezi kutibiwa hapa nchini, na gharama zote ikiwemo za kufuatilia hati ya kusafiria ni yeye anagharamia na safari hiyo imeelezwa itatumia zaidi ya Sh50, 000,’amesema.

Wakati Pili akithibitisha hilo, mama wa Hawa Ndagina Shabani amesema hana taarifa yoyote kwa kuwa Diamond hajawahi kuwasiliana naye tangu mtoto wake alipoanza kuumwa.

Amesema anachojua ni kwamba taratibu za kufuatilia hati za mtoto wake kwenda India zimeshaanza kufanyika japokuwa hajui ni nani anayegharamia yote hayo kwani shida yake sio kumjua bali ni mtoto wake atibiwe.

Baadhi ya watu walioona ujumbe huo akiwemo Boniface Sospeter, amesema “labda ungempatia hizo pesa mapema pengine asingeugua ila sio mbaya hata ilichokifanya ni jambo zuri maaana ndivyo ilivyo wengi husubiri uwapo na tatizo ndo watoe msaada,”ameandika.

Naye Sifia James, mkazi wa Ubungo, akizungumza na Mwanasoti,amesema Diamond akubali kuambiwa ukweli kwamba kutokana na ukaribu aliokuwa nao kwa Hawa lipaswa kuwa mtu wa kwanza kumpa msaada, na badala yake amesubiri watu wamemlaumu ndio anajitokeza huku akijigamba kwamba alikuwa akimsaidia kimyakimya na kuhoji siku zote alikuwa wapi hadi Hawa akufikia hali hiyo.

Doroth Bernard, ameshauri wasanii kuwa na upendo wa kweli mtu anapokuwa mzima na anapopata matatizo kwa kuwa kila binadamu ni hli ambayo anaweza kuipitia, na kuongez kuwa wale wenye hali nzuri ya kimaisha wajue kujitolea kumsaidia mwenzao ni moja ya sadaka pia.