Mapya yaibuka mkataba wa Morrison Simba

Thursday October 01 2020
morison pic

Klabu ya Yanga imeibua upya utata mwingine wa mkataba wa mshambuliaji Bernard Morrison wakidai hana mkataba halali na wekundu hao wa Msimbazi.

Akizungumza jioni ya Alhamis Oktoba Mosi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Frederick Mwakalebela amesema wakati klabu yao ikipokonywa haki ya umiliki wa Morrison wamebaini mapungufu makubwa katika mkataba wa mchezaji huyo na Simba.

Mwakalebela ambaye amekuja na nakala anayodai ya mkataba huo amesema sehemu zote za mkataba huo zimesainiwa na mchezaji huyo pekee hatua ambayo sio sahihi.

Amesema katika mkataba huo pia hauna sehemu iliyosainiwa na kiongozi yoyote wa bodi ya Simba lakini pia hauna saini ya shahidi.

Pia,amesema katika kila nakala imesainiwa na Morrison pekee bila ya upande wa pili hatua ambayo inaoonyesha watani wao hao hawakuridhia mkataba huo.

"Hatua mbaya zaidi mkataba huu umepelekwa TFF na kutumika katika mfumo wa usajili na kupelekwa Fifa," amesema Mwakalebela.

Advertisement

Aliongeza"Mtakumbuka TFF walitupokonya haki wakidai mkataba wetu ulikuwa na mapungufu sasa haya nayo watatuambia nini.Yanga tunasema tunaomba kuona hatua kama tulizochukuliwa sisi basi na hapa zitumike.

" Tunafahamu kwamba mchezaji ili awe sahihi kucheza Ligi anatakiwa awe na leseni ambayo inakuja kwa kujumuishwa kwa vitu vingi ukiwemo mkataba halali",amesema Mwakalebela.

 

Advertisement