Manji arudi rasmi Yanga

Muktasari:

  • BAADA ya siku 517 tangu Yusuf Manji alipotangaza kujiuzulu, ametangazwa kurudi rasmi Jangwani baada ya Kamati ya Uchaguzi wa klabu hiyo, kutoiweka nafasi ya uenyekiti kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi utakaofanyika Novemba 24.

HAKUNA kitu ambacho wanachama na mashabiki wa Yanga walikuwa wakikisubiri kwa hamu kama taarifa hii ya kurejea tena kwa Mwenyekiti wao, Yusuf Manji.

Hii ni kwa sababu ndani ya siku 517 ambazo ni sawa na mwaka mmoja na miezi minne na siku 29 zilizotimia leo Ijumaa, tangu Manji alipotangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo Mei 20, mwaka jana Yanga imekuwa ikiishi maisha ya kuungauunga.

Kitendo cha Yanga kuyumba kiasi cha kufikia kutemeshwa taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu Bara walilokuwa wakilishikilia mara tatu mfululizo, kiliwafanya watani zao wa Simba kuwacheka na kuwakejeli kila uchao na hasa walipoanza kutembeza bakuli.

Hata hivyo, kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, kilichokutana juzi Jumatano kimekata mzizi wa fitina baada ya kumrejesha kwa nguvu Manji katika nafasi yake, huku wakitangaza rasmi tarehe ya Uchaguzi wa kuziba nafasi ndani ya Yanga.

Kamati hiyo, iliamua kupanga Uchaguzi wao ufanyike Novemba 24 mwaka huu kwa kuziba nafasi za Makamu Mwenyekiti, iliyoachwa wazi na Clement Sanga aliyejiuzulu kama ilivyokuwa kwa Wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Wajumbe waliojiuzulu ni Salum Mkemi, Hashim Abdallah na Omar Saidi kutoka Zanzibar, huku ikielezwa Ayoub Nyenzi kwa kutohudhuria vikao mfululizo kimemvua sifa za kuendelea kuwa Mjumbe wa Kamati hiyo ya Utendaji.

Kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo imesisitiza kuwa kwenye uchaguzi wao mdogo utakaofanyika jijini Dar es Salaam, nafasi ya Mwenyekiti haitogombewa kwa kuwa Manji hajaondoka Yanga kama ambavyo inaelezwa.

Mmoja wa vigogo wa kamati hiyo ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake amelitonya Mwanaspoti kuwa, bado bilionea huyo yuko Yanga na kile kinachozungumzwa nje kuwa hayuko Yanga na wala hataki kujihusisha na masuala ya klabu hiyo siyo ya kweli.

“Uchaguzi huo utahusisha kuziba nafasi ya makaamu na utatumika kuziba nafasi za wajumbe wengine waliojizulu, niwatoe wasiwasi Wana Yanga kuwa Mwenyekiti bado yupo na nafasi yake haitogombewa,” alisisitiza kigogo huyo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alipoulizwa kuhusu suala hilo la Mwenyekiti, alisema ishu yote iko chini ya kamati ya uchaguzi ambayo imepewa baraka la kulizungumzia hilo.

“Siwezi kulisemea kamati, ila imekutana na kuweka mambo yote sawa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu na hata suala la Mwenyekiti wenyewe ndio watalizungumzia,” alisema Kaya.

Hata hivyo, mjumbe wa Kamati ya uchaguzi wa Yanga, Bakili Makele, alisema ufafanuzi wa zoezi la uchaguzi na lini uchaguzi utafanyika na sakata la Manji utatolewa kwenye mkutano wa Waandishi wa habari wakati wowote kuanzia leo Ijumaa.

“Mchakato wa uchaguzi umekamilika, kamati yetu imekamilisha kila kitu na siku si nyingi Mwenyekiti wa kamati ataweka wazi mchakato wote utakavyokuwa,” alisema.

“Tulichokuwa tunakisubiri ni Mwenyekiti wa Kamati (Sam Mapande) arejee kutoka nje ya nchi alikokwenda kwa masuala binafsi, lakini wakati wowote kuanzia sasa mambo yatakuwa wazi,” alisema.

IMEANDIKWA NA IMANI MAKONGORO, CHARITY JAMES NA KHATIMU NAHEKA