Man United wanamtaka Aubameyang, afunguka

Muktasari:

  • Aubameyang anasema kwamba Henry ndio sababu kubwa ya yeye kuamua kuchukua jezi yenye namba 14 baada ya kuona ile namba 7 aliyokuwa akiitaka, imeshachukuliwa na Henrikh Mkhitaryan.

LONDON, ENGLAND. MAMBO ni mengi, muda ni mchache. Ndio hivyo baada ya kuibuka kwa habari kwamba Manchester United sasa inamtaka supastaa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang.
Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer anaripotiwa kumtaka Aubameyang akimtazama kama ni mshambuliaji mbadala wa kwenda kuchukua nafasi ya Romelu Lukaku kama ataondoka kwenda kujiunga na Inter Milan.
Hata hivyo, Arsenal hawana sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya staa wao huyo aliyeshinda Kiatu cha Dhahabu msimu uliopita sambamba na wakali wawili wa Liverpool, Mohamed Salah na Sadio Mane baada ya kusema kwamba bado hajafikiria kuondoka Emirates.
Kichapo kutoka kwa Chelsea kwenye fainali ya Europa League iliibua mashaka kwamba huenda Aubameyang, aliyefunga mabao 32 kwenye michuano yote msimu uliopita angeshawishika kuachana na timu hiyo, lakini mwenyewe amesema bado yupoyupo sana tu akitaka kufuata nyayo za shujaa wake Thierry Henry, aliyekuwa klabuni hapo na kwamba pia alikuwa akivaa jezi yenye namba 14 mgongoni.
“Nilipenda muda wangu niliokuwa Dortmund, lakini Arsenal waliponitaka, nilifurahia sana changamoto mpya,” alisema.
“Siku zote nimekuwa nikiipenda Arsenal kwa sabbu ina historia kubwa na wachezaji wakubwa kama Thierry Henry. Alikuwa mfano rahisi kwa washambuliaji na kwa sababu na mimi nina kasi na nafunga mabao, hivyo siku zote nimekuwa nikiiga mambo yake."
Aubameyang anasema kwamba Henry ndio sababu kubwa ya yeye kuamua kuchukua jezi yenye namba 14 baada ya kuona ile namba 7 aliyokuwa akiitaka, imeshachukuliwa na Henrikh Mkhitaryan.

Aubameyang, 30, alinaswa na Arsenal Januari mwaka jana kwa ada ya Pauni 56 milioni na kuwa mchezaji ghali Emirates.