Mamia wajitokeza msiba Tigana

Muktasari:

Tigana alizaliwa mwaka 1970 Ilala mjini Dar es Salaam na amekulia Mtaa wa Saadani huku akisoma shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ambako ndiko alianzia soka kama kipa na baadaye mchezaji wa ndani.

Dar es Salaam. Wadau na mashabiki mbalimbali wa soka, wamejitokeza  Msasani ambako upo msiba wa nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Ally Yussuf   ‘Tigana’.
Miongoni mwa wadau hao wapo ambao wanaonekana kuvalia jezi ya Yanga  kama inshara ya kuomboleza kutokana na mapenzi mazito aliyokuwa nayo marehemu na klabu hiyo licha ya kutesa pia akiwa na Simba.
Rafiki wa karibu wa marehemu, Mwanamtwa Kihwelui ambaye alicheza naye soka  enzi za uhai wake, alionekana kuchakalika kuweka mambo sawa katika msiba huo.
Hata hivyo bado hawajaanza kuonekana wachezaji wa zamani ambao alitesa nao, viongozi wa klabu mbalimbali  za Ligi Kuu na hata wa shirikisho la soka nchini (TFF).
Wakina Mama na baadhi ya vijana wameonekana kuweka mambo sawa  upande wa mapishi ya chakula wakati huu wa mchana kabla ya kuanza kwa safari ya kwenda kumpumzisha Tigana.
Kiungo huyo  ambaye aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', amefariki dunia jana katika hospitali ya Amana mjini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa shemeji wa marehemu, Seleman Hamisi ambaye mke wake ni dada wa Tigana aitwaye Cheka, alisema wanatarajia kumpumzisha ndugu yao huyo leo  majira ya saa 10:00 katika  makaburi ya Msasani.
“Ameondoka ghafla kutokana na kusumbuliwa na tumbo. Umauti umemkuta akiwa Amana ambako alipelekwa kwa matibabu,” alisema Hamisi