Makocha 64 waomba kazi Yanga

Muktasari:

HUKO Yanga mambo yamezidi kunoga! Hadi sasa tayari kuna majina ya makocha 64 waliotuma maombi ya kazi ya kukinoa kikosi hicho.

HUKO Yanga mambo yamezidi kunoga! Hadi sasa tayari kuna majina ya makocha 64 waliotuma maombi ya kazi ya kukinoa kikosi hicho.

Si unakumbukua, Jumatatu ilikuwa siku mbaya kwa wapenzi wa Yanga baada ya kusikia matamshi yaliyotolewa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Luc Eymael juu ya kile alichoamini kukosa uvumilivu.

Hata hivyo, uongozi wa timu hiyo haukusita kumfuta kazi, Eymael kwa madai ya kauli zake za kibaguzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinus anasema saa chache tangu, Eymael afutwe kazi siku hiyo makocha nane walikuwa wametuma maombi ya kutaka kazi ya kuifundisha Yanga.

Aliongeza hadi sasa majina ya makocha 64 yametua ofisini wakiomba kazi na majina 12 ni makocha wazawa huku makocha wa kigeni wakionekana kumiminika zaidi ambao wengi wao ni kutoka nje ya Bara la Afrika.

“Mchakato huu utachukua wiki moja pekee ili kumpata kocha haraka na kuanza kazi ya kukiandaa kikosi kwaajili ya msimu ujao.

“Wachezaji wamepewa mapumziko ya wiki mbili, watakaporejea kambini watamkuta kocha amekwishapatikana, msimu ujao tunataka ubingwa,” alisema Albinus.