Makambo ashtukiwa Yanga

STRAIKA namba moja wa Yanga, Heritier Makambo ni kama ulivyosikia, jamaa ameanza kurudi kambani baada ya kukumbana na ukame wa muda mrefu, lakini kumbe kuanza kwake kutupia tena kumetokana na kikao flani alichofanya na kocha wake, Mwinyi Zahera.

Kocha Zahera alimshtukia Makambo ana kitu fulani tangu arejee kutoka DR Congo na fasta akaitisha kikao naye na kumpa kazi nzito.

Makambo kwa sasa ana mabao 12 baada ya bao alilofunga juzi dhidi ya Mbao FC lakini kumbe Kocha Zahera alimshtukia mapema kuwa tangu arudi kutoka Masina ndani ya Jiji la Kinshasa uwezo wake umepungua.

Zahera alisema aligundua Makambo ameongezeka uzito wa mwili kidogo kitu ambacho kimempunguzia wepesi wa kuwasumbua mabeki kisha akafanya naye kikao kifupi cha kumpa kazi ya kubadilika.

“Makambo hakuwa sawa kama yule aliyekuwa anafunga mabao 10 huko nyuma tangu arudi kutoka Congo hakuwa sawa niligundua ameongezeka uzito,” alisema Zahera.

“Nilikaaa naye tukazungumza hayo yote na kumtaka abadilike haraka apunguze uzito.”

Zahera alisema mbali na hilo pia alimtaka mshambuliaji huyo kama kuna mambo anayafanya nje ya uwanja ambayo hayana tija katika kipaji chake aachane nayo.

Alisema ingawa juzi alifunga lakini bado hajaridhika na kiwango chake akimtaka kuzidisha juhudi kurudi katika ubora wake.

“ Hajaanza kufunga jana (juzi) alifunga hata mechi mbili zilizopita, lakini walikataa bao lake, sijaridhika na kiwango chake, japo jana alifunga anatakiwa kujituma zaidi arudi katika ubora wake.”

TSHISHIMBI SAFI

Zahera akimgeukia kiungo wake Mkongomani, Papy Kabamba Tshishimbi alisema anaanza kurudi katika ubora wake.

Alisema Tshishimbi ameanza kuwa mtamu kwa kufanya yale ambayo amekuwa akimuagiza ayafanye uwanjani.

“Makambo sijawahi kuwa na tatizo naye kutokana na alikuwa na majeruhi sasa ameanza kurudi anacheza vizuri anafanya kile tunachotaka akifanye uwanjani naona atarudi haraka katika ule uwezo wake ninaoujua.

WAIFUATA NAMUNGO

Jana Alhamisi baada ya kurudi kila mchezaji akienda nyumbani kwake kupumzika lakini siku hiyohiyo jioni walitakiwa kukutana kwa maandalizi ya kuifuata Namungo FC ya Lindi katika mchezo wa Kombe la FA.

Mechi hiyo ya raundi ya tano itapigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Ilulu, mkoani Lindi huku pia kukiwa na michezo mingine siku hiyo ukiwamo wa African Lyon dhidi ya Mbeya City na Alliance itakayoikaribisha Dar City.

Lakini kabla ya mechi hizo za Jumapili, kesho Jumamosi zitapigwa mechi nne ikiwamo ya Kagera Sugar dhidi ya Boma FC, Lipuli itaumana na Dodoma, KMC itaikaribisha Mtibwa Sugar na kama vile haitoshi usiku Singida United itaialika Coastal Union Uwanja wa Azam Complex ambao Jumatatu utashuhudia wenyeji Azam ikipepetana na Rhino Rangers.