Mahadhi ruksa kukiwasha uwanjani

WINGA wa Yanga Juma Mahadhi aameanza mazoezi rasmi na kikosi hicho huku daktari wa timu hiyo Sheikh Mngazija akimuwashia taa ya kijani kuonyesha kuwa sasa kazi ni kwake tu kwani tayari amepona kabisa.

Mahadhi alikaa nje ya uwanja kwa mwaka mmoja na miezi tisa kutokana na kuwa majeruhi wa goti.

Aliumia goti katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Yanga  na USM Algiers ya Algeria uliofanyika Agosti  19, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuumia, winga huyo alifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Filbert Bay Kibaha lakini baadaye goti lilitunga tena usaha hivyo kufanyiwa upasuaji mwingine kwenye kitengo cha Mifupa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI).

Juzi Mahadhi alifanya mazoezi na wenzake kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria Ubungo yakiwa chini ya  kocha msaidizi Charles Mkwasa.

Katika mazoezi hayo  Mahadhi alionekana kwenda sawa katika kila mazoezi.

Mngazija alisema: “Ameshapona na hata hospitali alikokuwa anatibiwa wameshapewa ruksa ya kufanya mazoezi yoyote ila tu mwenyewe anakuwa muoga wakati mwingine kwa kuhofia labda anaweza kujitonyesha tena.

“Sasa hivi anatakiwa afanye mazoezi sana ili kurudisha nyama katika mguu wake kwani mara nyingi mtu yoyote ukifungwa bandeji ngumu (POP), ukija kutoa ngozi inakuwa kama imesinyaa.”