Macho kodo kwenye dili hizi saba kutiki

LONDON ENGLAND. DIRISHA la usajili wa Januari linazidi kunoga huku likibakiza siku chache tu kufika mwisho.

Mastaa kadhaa wameshuhudiwa wakihama kutoka timu moja kwenda nyingine, huku zikiwapo dili nyingine nyingi zinazodaiwa kwamba kuna uwezekano mkubwa zikatokea ndani ya mwezi huu ikiwamo ya straika wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta kwenda Aston Villa.

Hizi hapa dili saba zinazosubiriwa kwa hamu kuona kama zitakamilika ndani ya siku chache kabla ya dirisha la Januari kufungwa.

1. Layvin Kurzawa kwenda Arsenal

Layvin Kurzawa ameripotiwa kwamba yupo kwenye hatua za mwisho kabisa kutua kwenye kikosi cha Arsenal. Beki huyo wa kushoto wa Paris Saint-Germain anahitajiwa na kocha mpya wa kikosi hicho, Mikel Arteta akihitaji huduma yake kwenda kumaliza tatizo la mabeki linalosumbua kwenye timu yake. Beki huyo Mfaransa atakuwa mchezaji huru mwisho wa msimu, hivyo PSG watamwaachia tu sasa hivi.

2. Bruno Fernandes kwenda Man United

Bruno Fernandes kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na Manchester United. Kinachoripotiwa ni kwamba kuna mambo madogo tu yamechelewesha usajili huo huku Sporting Lisbon wakitaka wapewe mkwanja wote. Hata hivyo, dili hilo la kwenda Old Trafford ni kitu kinachosubiriwa kwa hamu na ni jambo linaloweza kutokea kwenye uhamisho wa mwezi huu wa Januari.

3. Christian Eriksen kwenda Inter Milan

Ripoti zinadai kwamba Inter Milan wanakaribia kukamilisha usajili wa kiungo Christian Eriksen. Staa huyo wa Tottenham amebakiza miezi michache wenye mkataba wake katika timu hiyo ya London, na kama hatauzwa dirisha hili basi ataondoka bure mwishoni mwa msimu. Kwa sasa Inter ndio wanatajwa kwamba wanaelekea kukamatia saini ya mchezaji huyo Januari hii.

4. Ross Barkley kwenda West Ham

West Ham United wanamtolea macho kiungo Ross Barkley wakimtaka kwa mkopo baada kocha David Moyes kutaka kuungana na mchezaji wake huyo wa zamani. Barkley mambo yake si mazuri huko Chelsea baada ya ujio wa kocha Frank Lampard, lakini Moyes baada ya kupata dili la kuinoa West Ham mpango wake ni kumchukua staa huyo aliyekuwa naye Everton.

5. Isco kwenda Chelsea

Kiungo huyo Mhispaniola anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji wanaocheza soka la kiwango cha juu sana huko Real Madrid chini ya kocha Zinedine Zidane. Lakini, kocha wa Chelsea, Frank Lampard ameripotiwa kusaka huduma ya fundi huyo wa mpira akimtaka atue Stamford Bridge ndani ya mwezi huu.

6. Bruno Guimaraes kwenda Arsenal

Arsenal wanahitaji huduma ya Bruno Guimaraes baada ya rais wa klabu anayocheza mchezaji huyo kuthibitisha hilo. Kocha Mikel Arteta anataka kukiboresha kikosi chake katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya baridi huko Ulaya ili kufanya timu kuwa imara katika kumalizika msimu. Sasa mpango wao ni kwenda kumsajili kiungo wa kati Mbrazili, Bruno Guimaraes kutoka Athletico Paranaense.

7. Ze Luis kwenda Tottenham

Tottenham Hotpur wapo sokonni kusaka mshambuliaji moto wa kuziba pengo la majeruhi, Harry Kane. Kocha, Jose Mourinho si mgeni kwa usajili na sasa akili yake ipo kwenye usajili wa straika wa Porto, Ze Luis ili kusaidia mambo walau hadi mwisho wa msimu. Mpango wa Spurs ni kumsajili mshambuliaji huyo mwenye miaka 28 kwa mkopo.