MO amliza Masoud,aanika dili Yanga

Muktasari:

  • Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma ambaye amepata dili mpya la kuinoa AS Kigali ya Rwanda, kutoacha kumwombea mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji 'Mo' ambaye pia ni mdhamini wa klabu ya Simba aliyetekwa wiki iliyopita ili apatikane akiwa salama.

IKIWA leo ni siku ya nane tangu mfadhili na mdhamini wa Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji, aliyekuwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma ameibuka akimlilia bilionea huyu, huku akifichua hakukuwa na dili lolote kati yake na klabu ya Yanga.

Masoud alisitishiwa mkataba wake ndani ya Simba ukiwa umesalia muda wa mwaka mmoja kwa kilichoelezwa kutoelewana na Kocha Mkuu, Patrick Aussems na kulikuwa na taarifa huenda akarejea nchini kujiunga na Yanga ama Coastal Union ya Tanga.

Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti kutoka Kigali, Rwanda Kocha Masoud alisema hakukuwa na kitu kama hicho na kama kweli kulikuwa na klabu zinazomtaka, basi hazikuwahi kuzungumza naye na kwamba kwa sasa ameshapata kazi Rwanda.

Masoud ambaye hajamaliza hata wiki mbili tangu Simba imvunjie mkataba alisema amelamba mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha AS Kigali inayoshiriki Ligi Kuu ya Rwanda ambayo msimu uliopita ilimaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara APR.

Masoud alisema amepewa shavu la kuinoa timu hiyo ambayo leo Ijumaa itatupa karata yake ya kwanza msimu huu, kuchukua nafasi ya Eric Nshimiyimana aliyejiuzulu.

Kocha Masoud aliyewahi kuifundisha Rayon Sports kabla ya kutua Simba alisema leo watavaana na Musanze FC, huku akisisitiza kuwa tangu aanze kufundisha soka miaka minne iliyopita alikuwa na hakika kutemwa kwake Simba kusingemfanya akose timu.

“Ni kweli nilizungumza na uongozi wa AS Kigali, tumekubaliana na mambo ni mazuri. Bado nahitaji kufundisha timu zaidi kwani nina muda mchache tangu nianze kufundisha, hivyo naona nina miaka mingi ya kuwa kocha kama Mungu atanipa uhai.

“Kuondoka kwangu Simba hakukumaanisha kwamba ndiyo mwisho wa safari yangu ya ukocha, hii ni mipango ya Mungu kwani unapoondoka sehemu moja Mungu anafungua milango mingine sehemu nyingine, hivyo nashukuru kwa hilo,” alisema Djuma.

AMLILIA MO

Aidha kocha huyo ameungana na wana Simba wengine wanaoendelea kumuombea Mungu bilionea wao, Mohammed Dewji aliyetekwa Alhamisi ya wiki iliyopita akidai ameshtuka sana kusikia taarifa hizo.

Kocha Masoud alisema kila Mtanzania na nchi jirani zisiache kuomba ili MO awe salama, akidai kuwa trukio hilo limemjeruhi moyo wake.

“Ni tukio la kusikitisha, tukio la kuumiza moyo, ila Watanzania na watu mbalimbali tusichoke kuomba Mungu ili huko aliko awe salama, naamini Mungu atamrejesha salama na hata vyombo vya dola vinafanyakazi zao kwa umakini mkubwa. Mungu amlinde Mo,”.

MO Dewji, ndiye mzabuni aliyeshinda kwenye mchakato wa uwekezaji ambapo alitangaza kuwekeza Sh 20 bilioni mara tu klabu hiyo itakapobalisha mfumo wa uendeshaji kutoka wanachama kwenda kampuni, mchakato ambao unaendelea sasa huku tajiri huyo akianza kufanya baadhi ya mambo ndani ya Simba ikiwamo kulipa mishahara wachezaji, ujenzi wa uwanja.

Baadhi ya wanachama wa Simba wamekuwa wakisoma dua ili kumuombea Mo Dewji na jana Alhamisi walikuwa nyumbani kwa Mmoja wa wazee wa klabu hiyo, Hamis Kilomoni ili kumlilia Mungu amnusuru bilionea na mfanyabiashara huyo maarufu.