MJIPANGE: Mbaraka amerudi upyaaa

AZAM FC wana kila sababu ya kucheka baada ya mtambo wao wa mabao, Mbaraka Yusuf kurudi tena uwanjani kufuatia kuwa majeruhi wa muda mrefu tangu walipomsajili akitokea Kagera Sugar. Mbaraka anakiri hakuna changamoto iliyompa wakati mgumu kama majeraha hayo ambayo yalimpata alipotua Chamazi na kushindwa kuendeleza moto aliyokuwa nao Kagera, akiwalaza njaa waliomuibua na kumtambulisha kwenye soka, klabu ya Simba.

Simba hawakuwa na hamu na Mbaraka, kwani licha ya kuwatungua uwanjani, pia aliwakata stimu walipodai kwamba ni mali yao baada ya kumpeleka kwa mkopo kwa Wakata Miwa wa Kagera.

Mshambuliaji huyo aliyetabiriwa kuwa tishio na kuibeba Tanzania, mambo yalimchachia alipotua Azam FC, lakini kwa sasa kila kitu kipo freshi na anasisitiza kuwa amerudi upya na wapinzani wake wajipange kwani amekuja kivingine akiisaka heshima yake.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na straika huyo kwenye mazoezi ya Azam yaliyofanyika Uwanja wa Azam Complex na kufunguka mengi kuanzia majeraha yake, safari ya Afrika Kusini na malengo yake katika soka. Ebu tiririka naye.

KUREJEA MAZOEZINI

Mtambo huo wa mabao wa zamani wa Kagera, anasema alianza mazoezi muda mrefu kabla ya mlipuko wa virusi vya corona na kwamba anatamani leo au kesho ligi ianze upya akinukishe.

“Baada ya ugonjwa ilibidi nipumzike nyumbani, lakini niliendelea na mazoezi binafsi, hadi sasa tulipoambiwa kuungana pamoja kujiandaa na Ligi Kuu na michuano ya Kombe la FA,” anasema.

Kama hujui ni kwamba tangu 2017 alipojiunga na Azam akitokea Kagera, Mbaraka alikumbana na majeraha yaliyomlazimisha awe nje kwa msimu mzima, lica ya kipindi flani kutolewa kwa mkopo Namungo FC alikoipandisha daraja.

CHANZO HIKI HAPA

Mbaraka anafichua kuwa majeraha yalianzia Namungo FC walipovaana na Mufindi United katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Anasemas alipata maumivu ya goti na hapo ndipo lilipoanzia tatizo lililomnyima raha.

“Baada ya majeraha nikauambia uongozi wangu wakafanya utaratibu wa matibabu, nikakaa nje mwaka mzima na ninawashukuru mabosi wangu wa Azam kwa kunitibia Afrika Kusini na kurejesha tumaini langu kisoka,” anasema.

AKIRI KUSHUKA KIWANGO

“Kiukweli nimeumia sana, kipindi niko Kagera na Azam, ni vitu tofauti. Kagera nilikuwa vizuri, ila Azam kama nimeshuka chini.”

Ila anasema kwa sasa yupo fiti na amepania kupambana kwa kila hali ili kurudisha kiwango chake kama alichokuwa nacho Kagera Sugar.

Mara kadhaa amekuwa akipewa moyo wa kupambana, licha ya changamoto za majeruhi alizokutana nazo. “Makocha wamekuwa wakinipa moyo, wanasema kikubwa nijikite zaidi kwenye nidhamu tu,” anasema.

AWATEGA WENZAKE

Mbaraka aliyetaka kurejeshwa Msimbazi, amepiga mkwara kuwa licha ya uwepo wa mastraika kadhaa kikosini Azam wakiwamo Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Shaaban Idd, ataendelea kuonyesha juhudi zote mazoezini.

“Naamini nikionyesha kiwango kizuri basi nitapata nafasi ya kucheza, kikubwa kujituma mazoezini ili kuwashawishi makocha.”

Kurejea kwake ni kama mtego kwa wenzake waliokuwa wakilibeba jahazi la Azam FC yaani kina Ngoma, Chirwa, Idd na Richard Djodi.

BAO BORA KWAKE

Mbaraka ametaja bao lake bora ambalo atalikumbuka muda wote kuwa aliwafunga Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Aprili 3, 2017 Uwanja wa Kaitaba, ambapo Simba ilipoteza kwa mabao 2-1.

“Nakumbuka ilikuwa Kaitaba nimepewa mpira nikageuka nikapiga shuti,” anasema Mbaraka. Katika mchezo huo bao la kufutia machozi la Simba lilifungwa na Mzamiru Yassin dakika ya 69. Mechi hiyo ndio iliyozua mzozo wa Simba kukata rufaa na kutaka wapewe ushindi wa mezani na kuitishia kwenda Fifa kwa madai kuwa beki Mohammed Fakhi alicheza akiwa na kadi tatu za njano.

NI ZAO LA SIMBA

Mshambuliaji huyo ni mmoja wa makinda wa Simba B waliounda timu kali ya vijana akiwa na kina Ramadhani Singano, Abdalah Seseme, Wiliam Lucian, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Hassan Isihaka na wengine chini ya kocha Seleman Matola na walifanikiwa kunyakua ubingwa wa Banc ABC kwa kuifunga Mtibwa.

Licha ya kuwa na mwanzo mzuri kwenye timu ya vijana ya Simba, Mbaraka alifanikiwa kupenya kwenye timu ya wakubwa wa Msimbazi kabla ya kushindwa kulishawishi benchi la ufundi la Simba.

Baadaye alitolewa kwa mkopo kwa Kagera Sugar na nyota yake kung’ara akifanya makubwa kiasi cha mabosi wake wa zamani kumtamani tena.

MGOGORO NA SIMBA

Licha ya Simba kumtaka kurejea Msimbazi baada ya kung’ara, kinda huyu aligoma kurudi akidai hana mkataba nao, huku Simba ikidai walikuwa na mkataba wa mwaka mmoja uliosalia. Jambo hilo liliibua mgogoro mkubwa kabla ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuingilia kati na kumtangaza kuwa mchezaji huru.

“Kiukweli sikuwa na mkataba wowote na Simba, nilitaka kuongeza mkataba, lakini ilishindikana kwani pesa waliyotaka kunipa ilikuwa ni ndogo, nilichokifanya nilichukua mkataba huo nikausome ila sikuurudisha,” anasema.

“Unajua waliweka pingamizi kwamba ni mchezaji wao, lakini huo wakati nilijitoa mhanga kuwa hata kama TFF wangesema nirudi Simba nisingeweza, nilikuwa tayari kukaa nje ya uwanja bila ya kucheza maana walichokuwa wakikifanya hakikuwa sawa.”

MAMBO YAKO HIVI

Mbaraka ana rekodi ya kipekee kwani amezifunga timu zake za zamani, Simba na Kagera Sugar kwa nyakati tofauti.