Liverpool na Spurs wanalisuta soka la Afrika

BAADA ya kupoteza mechi za kwanza za Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool na Tottenham Hotspurs wamepindua meza kibabe na kutinga hatua ya fainali katika namna ambayo wengi hawaamini hadi sasa.

Liverpool iliyokuwa imechapwa mabao 3-0 ugenini Hispania dhidi ya Barcelona, imetumia vyema mechi yao ya marudiano nyumbani England Jumanne wiki hii kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 ambao umewapeleka fainali.

Tottenham Hotspur ambayo ilitandikwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Ajax ya Uholanzi, imepata ushindi wa kibabe ugenini wa mabao 3-2 juzi Jumatano tena ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 baada ya wenyeji kutangulia kupata mabao ya mapema.

Kwa nini wengi wameshangaa kuona Liverpool na Tottenham zikigeuza matokeo na kufuzu hatua ya fainali licha ya kuonekana zina nafasi finyu ya kufanya hivyo baada ya matokeo ya mechi za mwanzo?

Ni kwa sababu hawajazoea kuona hali kama hiyo ikitokea barani Afrika hasa kwenye mashindano yanayohusisha klabu yaani yale ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Suala la kushinda ugenini au kupindua matokeo na kupata ushindi wa mabao mengi baada ya kuchapwa 3-0 nyumbani huku barani Afrika linaonekana kama maajabu na gumu kutokea.

Hii ni kwa sababu mpira wa Afrika umetawaliwa na fitina, hujuma na mipango ya timu mbalimbali hasa zile za Kaskazini mwa Afrika kwenye mataifa yanayozungumza Lugha ya Kiarabu.

Timu inapokwenda ugenini, itasumbuliwa kwenye Uwanja wa Ndege, itapuliziwa dawa ya kudhoofisha nguvu wachezaji hotelini, itapikiwa chakula kisichofaa, itarushiwa mawe na uwanjani mashabiki wa timu pinzani watawamulika na tochi za mionzi wachezaji huku pia marefa wakiibeba timu mwenyeji.

Lakini pia baada ya timu kushinda mabao 3-0 nyumbani huku Afrika, itaenda ugenini na kutumia muda mwingi kujiangusha na kupoteza muda badala ya kucheza mpira huku ikitumia mbinu nyingi za kuwatoa mchezoni wapinzani wao.

Kama soka la Afrika lingeendeshwa kwa usawa na haki pamoja na uwazi wa hali ya juu kama wanavyofanya Ulaya, ni wazi kwamba tungeshuhudia mara kwa mara aina ya matokeo ambayo Liverpool na Tottenham wameyapata kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini kwa mfumo uliopo sasa wa hujuma, fitna na ubabaishaji ambao unaendesha soka la Afrika, tutaendelea kuona matokeo ya namna hiyo kama jambo la kushangaza.

Wakati umefika sasa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kufumua mfumo wa uendeshaji wa mashindano yake na kuiga kile kinachofanywa na wenzetu wa Ulaya ili soka la Afrika liweze kupiga hatua.

Lakini kama hatutoona maana na umuhimu wa kile ambacho wenzetu wanakifanya, tutaendelea kuwa wasindikizaji na ndiyo maana hata klabu zetu zinapokwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia, zinajikuta zikifungwa hadi na timu za kutoka Saudi Arabia.