Lampard amtaka Drogba kwenye benchi Chelsea

Muktasari:

Na ripoti zinadai kwamba Lampard anamtaka Drogba aende akawe kocha wa washambuliaji kwenye kikosi chake na Shay Given anaweza pia kuhama kutoka Derby kwenda kuwa kocha wa makipa.

LONDON, ENGLAND.FRANK Lampard anaripotiwa kwamba amebakiza mambo machache tu kabla ya kuchaguliwa kuwa kocha mpya wa Chelsea na mpango wake ni kumwongeza Didier Drogba kwenye benchi lake la ufundi.
Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea, Lampard alicheza mechi zaidi 700 katika klabu hiyo, anatajwa kwamba atatua Stamford Bridge baada ya Maurizio Sarri kutimkia Juventus.
Kwa mujibu wa The Sun, mazungumzo yameendelea hadi Ijumaa baina ya Lampard na Chelsea kuhusu kumaliza suala la ukocha, huku The Blues wakiwa na kazi ya kuilipa Derby fidia ya Pauni 4 milioni ili kumpata kocha huyo.
Na ripoti zinadai kwamba Lampard anamtaka Drogba aende akawe kocha wa washambuliaji kwenye kikosi chake na Shay Given anaweza pia kuhama kutoka Derby kwenda kuwa kocha wa makipa.
Msaidizi wake Jody Morris naye amepanga kumtaja kwenye benchi lake la ufundi atakapotua Stamford Bridge, huku akiwatosa John Terry, ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi huko Aston Villa, iliyopanda daraja na kucheza Ligi Kuu England msimu ujao.
Jambo hilo pia linamweka kwenye wakati mgumu msaidizi namba mbili wa Sarri, Gianfranco Zola kuhusu hatima yake kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge.