Lampard: Bayern ni funzo tosha kwa Chelsea

Muktasari:

Chelsea ilijikuta ikimaliza pungufu baada ya Marcos Alonso kuonyeshwa kadi nyekundu huku kiungo wao wa kutegemewa Jorginho akionyeshwa kadi ya njano ya kizembe baada ya kubishana na mwamuzi hivyo nyota hao watakosekana katika mchezo wa marudiano.

London, England. Kocha wa Chelsea, Frank Lampard amesema kipigo cha mabao 3-0 ambacho wamekumbana nacho wakiwa nyumbani kutoka kwa Bayern Munich katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ni somo tosha kwa vijana wake.

Lampard alisema wapinzani wao walikuwa katika kiwango bora zaidi hivyo wachezaji wake wanatakiwa kutafsiri kipigo hicho kama somo ambalo litawasaidia katika mchezo wa marudiano nchini Ujerumani.

"Tulitakiwa kufanya zaidi. Siwezi kusema kuwa mchezo umemalizika kutokana na matokeo yalivyokuwa, kufungwa ni somo kali ambalo tunatakiwa kujua tunakazi kubwa ya kufanya mbele yetu.

"Hii ni Ligi ya Mabingwa hata kiwango cha ushindani huwa tofauti hasa katika hatua ya mtoano. Walikuwa bora karibu katika kila idara," alisema kocha huyo, alipokuwa akifanyiwa mahojiano na BT Sports.

Dakika tatu zilitosha kwa mshambuliaji wa Serge Gnabry kuitanguliza Bayern katika mchezo huo mwanzoni mwa kipindi cha pili na kuishuhudia miamba hiyo ya soka la Ujerumani ikiumiliki mchezo kabla ya Robert Lewandowski kupachika bao la tatu.

Chelsea ilijikuta ikimaliza pungufu baada ya Marcos Alonso kuonyeshwa kadi nyekundu huku kiungo wao wa kutegemewa Jorginho akionyeshwa kadi ya njano ya kizembe baada ya kubishana na mwamuzi hivyo nyota hao watakosekana katika mchezo wa marudiano.

Kwa Jorginho ni kutokana na kuonyesha kadi za njano mbili katika michezo mfululizo.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Gnabry ambaye aliwahi kuichezea Arsenal, alisema uwepo wa marafiki zake kwenye uwanjani, Stamford Bridge  ulimfanya kuwa na shauku ya kupachika mabao.

"Nina marafiki wengi hapa na walikuwa jukwaani hivyo sikutaka kuwaangusha," alisema na kuendelea kuuzungumzia mchezo huo, "Niliona vile ambavyo Liverpool walivyopindua matokeo msimu uliopita, bado tunakazi ya kufanya katika mchezo wa marudiano."

Upande wake kocha wa Bayern Munich, Hans-Dieter Flick alisema, "Ni kweli tumepata matokeo mazuri na niwapongeze wachezaji wangu kwa sababu umecheza vile ambavyo tulijiandaa."