Lacazette amchapa Lukaku

Muktasari:

Mshambuliaji Lacazette ameanza msimu huu kwa kishindo akiwa amezifumania nyavu mara nne na kutegeneza mawili tofauti na Lukaku ambaye bado mambo magumu kwake

LONDON, ENGLAND. Hivi unaijua hii? Alexandre Lacazette anamchapa Romelu Lukaku huko kwenye Ligi Kuu England.

Huu ni mwaka wa pili kwa Lacazette kwenye ligi hiyo, wakati Lukaku ni mwaka wa saba, lakini kwa msimu huu huduma ya fowadi huyo Mfaransa imekuwa na maana zaidi kuliko ya Lukaku.  Hapo ndipo anapomchapa!

Ni hivi, Lacazette akiwa na jezi za Arsenal msimu huu ameshahusika kwenye mabao sita, akifunga manne na kuasisti mara mbili.

Lacazette amefanya hayo baada ya kuwa uwanjani kwa dakika 536 tu, huku mabao yake aliyofunga, akiwa amefanya hivyo kila baada ya dakika 134. Lukaku, amehusika kwenye mabao manne tu, ambayo ndio aliyofunga na hajatoa asisti yoyote.

Kwa mabao hayo manne, Lukaku alihitaji dakika 653 za kuwa uwanjani, ikiwa ni zaidi ya dakika 117 ukilinganisha na zile za Lacazette, ambaye amehusika kwenye mabao mengi zaidi, sita. Takwimu hizo, Lukaku amefunga bao moja kila baada ya dakika 163.

Kwa rekodi za ufungaji kwenye ligi ya msimu huu, Manchester United inapaswa kujitazama mara mbili, hakuna maajabu kama itaendelea kutumia huduma ya fowadi huyo.

Lukaku amechapwa hadi na Pierre-Emerick Aubameyang, ambapo staa huyo wa Arsenal amehusika kwenye mabao matano katika ligi na alihitaji dakika 587 tu ndani ya uwanja kufanya hivyo.

 Fowadi huyo wa Man United amezalilishwa zaidi na Eden Hazard licha ya yeye kucheza zaidi karibu na goli la wapinzani. Kwa msimu huu kwenye ligi hiyo, Hazard amehusika kwenye mabao 10, akifunga saba na kuasisti mara tatu.

Lakini Hazard amefanya hivyo kwa kutumia dakika 577 tu alizokuwa ndani ya uwanja. Kumbuka Lukaku ametumia dakika 653 na kuhusika kwenye mabao manne tu.

Kwa Lukaku hakuna maajabu, kwani amezidiwa hadi na Sergio Aguero, ambaye amehusika kwenye mabao saba, akifunga mara tano na kuasisti mawili baada ya kutumia dakika 582 tu uwanjani.

Fowadi huyo wa Kiargentina, Aguero naye muda wake uko chini ukilinganisha na Lukaku, huku akiwa amehusika kwenye mabao mengi zaidi.

Harry Kane, amehusika kwenye mabao sita, akifunga matano na kuasisti moja huku akitumia dakika 718 ndani ya uwanja. Amezidi Lukaku dakika 65, lakini fowadi huyo wa Tottenham Hotspur, amehusika kwenye mabao mawili zaidi ya Lukaku. Kufunga mabao mawili, Lukaku anahitaji dakika 326 kwa wastani wake wa sasa.

Hivi ndivyo, fowadi huyo wa Man United anavyochapwa na wenzake kwenye Ligi Kuu England.

Kwa rekodi hizo zinamfanya Lukaku kuwa na wastani mdogo sana wa kushinda Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England msimu huu kama ataendelea kwa mwendo huo wa kinyonga kwenye kufunga, bao moja kila baada ya dakika 163 si kasi inayovutia, ndio maana kwa sasa Man United inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 13 na mabao yao 13 ya kufunga, huku ikiwa imefungwa 14. Ni aibu!