Kurasini Heat, Vijana zasaka tuzo NBL

Muktasari:

Ligi hiyo iliyoshirikisha timu 11 itafikia tamati leo jioni kwa mchezo wa fainali kati ya Kurasini Heat na Oilers.

chana na fainali ya Ligi ya Taifa ya mpira wa kikapu itakayopigwa leo saa 10 jioni kati ya Kurasini Heat na Oilers, timu hizo sanjari na ile ya Vijana na Don Bosco Panthers zinachuana kusaka tuzo msimu huu.

Oilers itacheza na Kurasini Heat kusaka ubingwa wa msimu huu kwenye uwanja wa Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam saa 10 jioni leo Jumapili Oktoba 25, 2020 huku Vijana ikicheza na Don Bosco Panthers kusaka mshindi wa tatu.

Mbali na mechi hizo za kuamua bingwa, nyota wa Vijana, Fotius Felesian na Gwalugwano John wanachuana kusaka tuzo ya mzuiaji bora (blocker).

Mpaka sasa wachezaji hao kila moja amezuia mara saba, licha ya kwamba wanapewa presha na Ally Buluba wa Don Bosco Panthers ambaye amezuia mara 5 na baadae ataiongoza timu yake katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu.


Jonas Mushi wa Vijana aliyefunga pointi 112 yuko kwenye rada za kusaka tuzo ya mfungaji bora msimu huu, licha ya kupewa presha na Brian Muramba wa Don Bosco Panthers aliyefunga pointi 96 na Joseph Kamanda wa Oilers mwenye pointi 93 na wote watacheza mechi zao za mwisho baadae jioni ya leo Jumapili.

Katika tuzo ya mchezaji aliyefunga mitupo mitatu (three pointer), Sylvian Yunzu wa  Don Bosco Panthers ndiye kinara akiwa amefunga mara 14 ingawa anapewa presha na Mushi aliyefunga mara 10 sawa na Joas Maheta wa Savio na Philbert Mwaipungu wa ABC ambao timu zao zimeondoshwa mashindanoni.

Sylvian Yunzu wa Don Bosco Panthers naye anawania tuzo ya mchezaji aliyetoa pasi za mwisho (Assister) mara nyingi zaidi akiwa ametoa mara 19, akifuatiwa na Josephat Peter wa Pazi ambaye ametoa mara 18 ingawa timu yake imeondoshwa mashindanoni na Amin Mkosa aliyea assist mara 16 na Fadhil Chuma mara 15 wote wa Kurasini Heat.

Fotius Felesian wa Vijana anawania tuzo ya mchezaji aliyeokoa mipira ya mwisho (Rebounder) mara nyingi zaidi akiwa amechukua mara 52 akipewa presha na Maxwell Ngonga wa Oilers aliyeokoa mara 48.