Kuna mtu ataumia

Saturday September 19 2020

 

By IMANI MAKONGORO

KWA rekodi za mechi Kagera na Yanga mjini Bukoba pamoja na jinsi Makocha na wachezaji wa timu hizo walivyopania, kuna mtu ataumia mapema tu.

Yanga itakuwa ugenini leo Jumamosi kucheza mechi yake ya kwanza msimu huu ikiwa na sura nyingi mpya sawa na Kagera ya Kocha Mecky Maxime ambaye alichomoa mpango wa kuwa Kocha Msaidizi wa Yanga dakika za mwisho kabla ya msimu kuanza.

Licha ya msimu uliokwisha Yanga kukubali kipigo cha mabao 3-0 ikicheza nyumbani Dar es Salaam Januari 3, 2020, mabingwa hao wa kihistoria lakini walichukua pointi tatu ugenini Julai 8 ingawa hawakuweza kulipa idadi hiyo ya mabao katika mchezo wa marudiano kwenye uwanja wa Kaitaba, Yanga ilipochomoza na ushindi wa bao 1-0.

Licha ya nyota wake wapya kama Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Michael Sarpong, Yacouba Sogne na Carlinhos ambao kwa mara ya kwanza watacheza kwenye Uwanja wa Kaitaba, rekodi za misimu mitano ya Ligi zinaibeba Yanga.

Katika misimu mitano, Yanga imeifunga Kagera mara tisa, huku kipigo kikubwa zaidi kuiadhibu timu hiyo Kaitaba kikiwa cha mabao 6-2 Oktoba 22, 2016.

Kagera yenyewe katika misimu mitano, imeifunga Yanga mara moja Jan 3, 2020 na kuweka rekodi ya kuichapa kipigo kikubwa Yanga nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Advertisement

REKODI HIZI HAPA

Oktoba 31, 2015, Kagera ikicheza nyumbani ilikubali kipigo cha mabao 2-0, kabla ya kuendeleza uteja kwa Yanga Aprili 2, 2016 kwa kipigo cha mabao 3-1, Dar es Salaam.

Oktoba Oktoba 22, 2016, Kagera iliduwazwa na Yanga kwa kipigo cha mabao 6-2 mjini Bukoba na Aprili 13, 2017 ikaruhusu kipigo kingine cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa marudiano.

Oktoba kwa mara ya tatu uliendelea kuwa mchungu kwa Kagera Sugar kwenye uwanja wao wa nyumbani, ambapo Oktoba 13, 2017 waliruhusu kipigo kingine cha mabao 2-1 na Machi 7, 2018 wakafa Taifa kwa mabao 3-0.

Msimu wa 2018/2019, Kagera tena ilianza kwa kipigo cha mabao 2-1 nyumbani Agosti 25, 2018 na kipigo kingine cha mabao 3-2 Januari 8,2019 jijini Dar es Salaam.

Kagera iliwalaza Wananchi na viatu msimu wa 2019/2020 baada ya kuwaadhibu kwa kipigo cha mwaka cha mabao 3-0 Januari 3, 2020 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ingawa Yanga ilijipooza kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 kwenye mchezo wa marudiano mjini Bukoba Julai 8.

Msimu mpya wa Ligi pia rekodi inaibeba zaidi Yanga ambayo ina pointi nne katika mechi mbili ilizokwishacheza, imetoka sare moja na kushinda moja.

Kagera yenyewe imefungwa mechi moja na kutoka sare moja ikiwa na pointi moja katika mechi mbili.

MAKOCHA WATAMBA

Kocha wa Yanga, Zlatko Krmpotic, raia wa Serbia amesisitiza kutaka pointi tatu katika mchezo huo; “Tunaamini tutafanya vizuri, tuna ari na morali ya ushindi na kuchukua pointi tatu na kuanza vizuri mechi yetu ya kwanza ugenini.”

Kocha mzawa, Mecky Mexime wa Kagera Sugar alisema; “Tutapambana kusaka matokeo, tutacheza kwa tahadhari na kuhakikisha tunatimiza mipango yetu ya kubakisha pointi tatu nyumbani.”

Ally Mayay ambaye ni mchambuzi wa habari za soka na pia mchezaji wa zamani wa Yanga, alisema pamoja na Kagera Sugar kuwa bora ikiwamo msimu uliopita kuifunga Yanga nyumbani, lakini mabingwa hao wa kihistoria wa msimu huu ni bora zaidi ya wa msimu uliopita.

“Bahati nzuri Uwanja wa Kaitaba unaruhusu kucheza mpira wowote kwani ni wa nyasi bandia na Mecky falsafa yake ni kuchezea mpira na viungo wenye ubora huo anao, hivyo mechi ya kesho (leo) itakuwa inashindanisha mbinu za Kagera na vipaji binafsi vya Yanga,” alisema.

Advertisement