Kumbe ni mpango Djuma kutimulia Simba!

Monday October 8 2018

 

By Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Kitendo cha timuatimua ya makocha wakuu na wasaidizi wao ndani ya kikosi cha Simba kwa haraka unaweza kusema kama zengwe fulani hivi.

Hii ni kutokana na nanma wanavyoondoka, kuna kipindi makocha wasaidizi wanaonekana kuwa na nguvu na baada ya muda na wenyewe hutimuliwa na kuwaacha wakuu wao wakitamba.

Tathmini ya kipindi cha takribani misimu  minne hivi, chini ya wasaidizi, Seleman Matola, Jackson Mayanja raia wa Uganda na Mrundi Masoud Djuma kutokana na namna walivyofanya kazi na wakuu wao.

 

MATOLA NA KERR

Ngoma ilianzia kwa Kocha Seleman Matola ambaye kwa sasa anaifundisha klabu ya Lipuli FC ya mkoani Iringa.

Advertisement

Matola alikuwa kipenzi wa mashabiki wa Simba na ishu yake ilianzia kwa Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic 'Loga'.

Walifanya kazi pamoja lakini baada ya muda, Loga alionekana hana mpya na hafai ndani ya kikosi hicho sababu ikiwa ni kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, alitimuliwa na Matola akabaki.

Inadaiwa kuwa, safari ya Loga aliyetimkia Kenya haikuwa ubingwa tu bali Matola ambaye alikuja kuwa mwenyeji wa Dylan Kerr.

Wakiwa kazini pamoja, hali ya sintofahamu ilizuka kwa wawili hao, ambapo ilidaiwa kuwa Matola ndiye alikuwa akilalamika hapati ushirikiano kutoka kwa mkuu wake huyo.

Mwisho wa siku, Matola mwenyewe  aliamua kuondoka na akamwacha Kerr akitamba.

Lakini, Kerr alitafutiwa msaidizi wake ambaye ni Jackson Mayanja raia wa Uganda na kuendelea kufanya naye kazi.

Wakiwa kazini, Mayanja na Kerr ambaye sasa anaifundisha Gor Mahia ya Kenya. Likazuka jambo la sintofahamu kati ya Mzungu huyo mzaliwa wa Kisiwa cha Malta nchini England na Mayanja.

Hali haikuwa nzuri na badaye, Kerr alitimuliwa kwa madai ya kushindwa kutimiza makubaliano ya mkataba na mabosi wake.

 

MAYANJA NA OMOG

Baada ya kuondoka, Mayanja aliendelea kuinoa Simba na akatafutiwa mkuu wake mwingine ambaye ni Mcameroon Joseph Omog kocha aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara Azam FC msimu wa 2013-2014.

Baada ya Omog kutua, kulizuka maneno kuwa Mayanja hataki kufanya kazi Simba kama kocha msaidizi lakini baadaye ikajulikana ni maneno tu kwa sababu alikuja na wakawa kitu kimoja.

Wakiwa kazini baada ya muda kupita, Mayanja ndiye aliomba kuondoka Simba kwa sababu ya majukumu yake binafsi na akaamua kurudi kwao Uganda.

Baada ya kufanya hivyo, alimwacha Omog ndani ya timu peke yake na baada ya muda akaletewa Masoud Djuma na kuanza kufanya naye kazi.

Lakini, wakiwa kazini ndani ya kipindi cha takribani nusu msimu, liakaanza zengwe la maana na hapo Omog alionekana hafai na hana mpya.

Licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa, upepo ulikuwa kwa Djuma ambaye alioneka bora zaidi ya Omog ambaye baada ya muda alitimuliwa kazi.

Sababu haikujukana wazi ilielezwa timu haichezi vizuri na mambo mengine.

 

DJUMA NA AUSSEMS

Kuondoka kwa Omog ndipo Simba waliamua kumleta Mfaransa Pierre Lechantre na kuchukua mikoba yake lakini hata hivyo hakudumu aliondoka kwa madai ya mkataba.

Lakini, ukweli wa mambo kinachodaiwa ni Djuma. Lechantre alionekana hana kitu mbele ya Mrundi huyo aliyeifundisha kwa mafanikio klabu ya Rayon Sports ya Rwanda.

Djuma alikuwa na nguvu kwenye timu na aliwashika kweli wadau na mashabiki wa Simba wakiamini hakuna mwingine isipokuwa yeye tu.

Kuondoka kwa Lechantre ndipo Aussems akaletwa kuingoza Simba. Lakini, ikiwa hata nusu ya msimu haujapita kukazuka zengwe la namna hiyo kuwa, hakuna maelewano baina ya wawili hao na ndipo, Djuma akafungashiwa vurago vyake.

Aussems na Djuma walianza kufanya kazi pamoja Julai mwaka huu katika maandalizi yao nchini Uturuki.

Na kuondolewa kwake ni malalamiko ya Aussems kwa madai hana imani na msaidizi wake.

Advertisement