Kumbe Barca imepiga kimyakimya kwa Kane

Thursday May 21 2020

 

BARCELONA, HISPANIA. NDO hivyo. Barcelona imeripotiwa ilibisha hodi Tottenham Hotspur kwenda kuulizia uwezekano wa kumsajili straika Harry Kane kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.

Licha ya kuwa na mkataba mrefu huko Spurs, miamba hiyo ya London imekuwa na wasiwasi juu ya kumbakiza mchezaji huyo kwenye kikosi chao kutokana na kuhusishwa na mpango wa kuondoka, huku mwenyewe akidaiwa kuwapa masharti mabosi wa timu yake kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya kimaendeleo, basi anakusanya virago vyeka.

Wakati sasa klabu zikitikiswa kiuchumi na kutokuwa na uhakika wa kufanya matumizi makubwa kwenye soka, Barcelona inaripotiwa ilikuwa tayari kutoa mkwanja mrefu kunasa saini ya Kane mwaka jana.

Hata hivyo, taarifa za kutoka Hispania zinafichua Barcelona hawakuonyesha uhitaji mkubwa sana katika kunasa saini ya mfungaji huyo wa England na ndio maana dili hilo lilishindwa kukamilika.

Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu aliripotiwa kufanya mawasiliano na mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy na kuzungumza kabla ya wawili hao kushindwa kufikia kwenye makubaliano ya mwisho.

Kane, mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa, amejifunga kwenye kikosi cha Spurs akiwa na mkataba hadi mwishoni mwa msimu wa 2023-24.

Advertisement

Straika Kane pia amekuwa akihusishwa na Manchester United wakiripotiwa kuhitaji saini yake kwenda kuongoza safu ya ushambuliaji huko Old Trafford, ambayo kwa sasa haina mtu wa maana baada ya kuondoka kwa Romelu Lukaku.

Advertisement