Kumbe Auba kaitosa Barca

 LONDON ENGLAND. STRAIKA, Pierre-Emerick Aubameyang amethibitisha kugomea ofa kibao za klabu nyingine ikiwamo Barcelona ili tu abaki Arsenal na kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye klabu hiyo ya London.

Manchester United nao walihitaji huduma ya nahodha huyo wa Arsenal, ambaye mkataba wake mpya aliosaini kwenye kikosi hicho cha Emirates wa muda wa miaka mitatu unamshuhudia akilipwa zaidi ya Pauni 350,000 kwa wiki.

Aubameyang alisema Kocha Mikel Arteta pamoja na mashabiki ndio watu waliomfanya atupilie mbali ofa ya Barcelona na kuamua kubaki zake kwenye kikosi cha Arsenal.

“Kulikuwa na ofa nyingi sana, hasa ya kutoka Barcelona na klabu nyingine,” alisema.

“Suala langu la kubaki lilisababishwa na mambo mawili. Kwanza Kocha Mikel Arteta na pili ni mashabiki.”

Sambamba na hilo, Aubameyang ameitaka klabu hiyo kuhakikisha inafanya usajili wa kiungo mchezeshaji Houssem Aouar kutoka Lyon kabla ya dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi kufungwa Oktoba 5.

Arsenal imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumnasa kiungo huyo wakiweka mezani ofa ya Pauni 34 milioni, lakini klabu hiyo ya Ufaransa inamthaminisha nyota wao kuwa na thamani ya Pauni 45 milioni.

Kuhusu Aouar, Aubameyang alisema:

“Ni mchezaji mzuri sana. Nadhani tutakuwa wenye bahati tukipata wachezaji wa aina hii kwenye klabu yetu. Ataleta mambo mengi sana mazuri.”