#Kuelekea Uchaguzi Mkuu Simba: Huyu ndiye Said Tulliy

Muktasari:

  • Uchaguzi wa Simba utafanyika Novemba 4, ambako wanachama watachagua uongozi mpya wa kumaliza miaka minne ya utawala wa rais Evans Aveva

SAID Tulliy ni mmoja ya wagombea 17 wa Ujumbe kwenye Uchaguzi Mkuu wa Simba. Mgombea huyo alizaliwa Oktoba 13, 1976, jijini Dar es Salaam. Aliwahi kuzichezea klabu za Dar Fire FC iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Tatu mwaka 1995 –2000,
Mwaka 2000 –2002 alijiunga na Coastal Union ya Ligi Kuu Bara ambapo mwaka
2002/03 alijiunga na Township Rollers FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Botswana timu hiyo ikiwa chini ya kocha Ramadhan Nswanzurwino wa Mbeya City.
Mwaka 2005/09 alijiunga na timu ya Banki ya Malaysia FC iliyokuwa inashiriki ligi daraja la tatu na kabla ya kujiunga na klabu hiyo 2007/08 aliitumikia Ashanti United akiwa Mratibu wa timu.
Mwaka 2008/09, Tulliy alikuwa Mkurugenzi wa Moro United na kuwa Mratibu wa Taifa Cup wilaya ya Ilala mwaka 2007/10.
Tulliy aliingia rasmi ndani ya Simba 2010/12 akiwa Mjumbe wa Kamati ya Ufundi/Usajili ambapo mwaka 2013/15 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Soka la Vijana ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Katika uchaguzi wa mwaka 2014 ambao uongozi wake umemalizika mwaka huu, Tulliy alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba chini ya Rais Evans Aveva.
Hivi sasa, Tulliy anagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambao wataingia moja kwa moja kwenye Bodi ya Wakurugenzi mara baada ya klabu hiyo kubadilisha mfumo wa uendeshaji kutoka klabu ya wanachama kwenda Kampuni.