#Kuelekea Uchaguzi Mkuu Simba:Ally Suru kumbe si mchezo

Muktasari:

  • Uchaguzi wa Simba utafanyika Novemba 4, ambako wanachama watachagua uongozi mpya wa kumaliza miaka minne ya utawala wa rais Evans Aveva

BAADA ya kumalizana na wagombea wa nafasi ya Uenyekiti, jana Alhamisi tukimalizia kwa Mteni Ramadhani baada ya awali kuanza na Swedio Mkwabi, leo tunawageukiza wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika Uchaguzi Mkuu wa Simba.

Uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 4, unashirikisha jumla ya wagombea 19, wawili wakiwa ni wanaowania Uenyekiti na waliosalia ni Wajumbe na kama kawaida Mwanaspoti inaendelea kuwaletea wasifu wa wagombea wa kinyang'anyiro hicho.

Lengo la kurasa hii ni kutaka kuwatambulisha wagombea hao kwa wanachama wa Simba kwa wasifu wao kabla ya kuanza kwa kampeni zilizopangwa kufanyika Okt 26 hadi Nov 3, ambapo watajinadi kwao ili kuwashawishi wawapigie kura kuwachagua.

 

ALLY SURU

Suru alikuwemo uongozi uliopita akiwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, ni mbobevu wa mahesabu kwani ni Mhasibu wa ngazi ya juu.

Suru ana shahada ya Uzamili ya Ununuzi na Ugavi aliyoipata katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Shahada ya Juu ya Uhasibu (CPA), Shahada ya Uzamili ya Fedha na Uwekezaji (Chuo Kikuu cha Coventry).

Ana Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Fedha (Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Shahada ya Uhasibu ambayo pia aliipata katika chuo cha IFM huku elimu ya Sekondari aliipata shule ya Sekondari ya Mazengo (Kidato cha kwanza hadi nne), Kidato cha tano na sita akiipata shule ya sekondari Makongo.

Suru alianza kuwa kiongozi wa michezo katika Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), alikuwa kiongozi wa mpira wa miguu (Kamati ya Olimpiki), Club Licensing (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika-CAF).

Uzoefu kwenye michezo, alikuwa Mbunge Serikali ya Wanafunzi (IFM), Makamu Mwenyekiti Kamati ya Michezo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwenyekiti  Kamati ya Michezo Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Mjumbe Mkutano Mkuu SHIMIWI Taifa.

Ndani ya Simba, Suru alikuwa na vyeo vifuatavyo, Mjumbe Kamati ya Maendeleo Soka la Vijana, Mjumbe Kamati ya Masoko na Uwekezaji, Mjumbe Kamati ya Fedha, Mjumbe Kamati ya Utendaji na Mjumbe Bodi ya muda ya Wakurugenzi.