Koulibaly huyo hapo jibebeeni

LONDON, ENGLAND. FRANK Lampard ameripotiwa kuwa na mpango wa kuongeza sura mpya kwenye kikosi chake cha Chelsea huku jambo hilo likiwafanya kuhusishwa zaidi na masupastaa, Jadon Sancho na Philippe Coutinho.

Bosi huyo wa The Blues anataka kufanya maboresho kwenye kikosi chake baada ya kupita madirisha mawili ya usajili bila ya kunasa staa mpya, huku hivi karibuni walifanikiwa kumnasa winga wa Ajax, Hakim Ziyech pekee.

Kwa sasa ataendelea kubaki na wachezaji wake makinda wakati msimu wa Ligi Kuu England utakapoendelea, lakini mara utakapokwisha tu na dirisha la usajili kufunguliwa basi atahitaji sura mpya chache kwenye chama lake hilo.

Lakini, kuhusu Sancho, wapinzani wao Manchester United ndio wanaonekana kuongoza kwenye mbio za kumsajili Mwingereza huyo, hivyo wanafahamu itakuwa shughuli pevu kwenye mapambano hayo huku ishu ya Coutinho nayo ikiwa na upinzani mkali kutokana na Arsenal kuonekana kuhitaji huduma yake pia.

Sura nyingine mpya anazozisaka Lampard ni beki wa kushoto wa Leicester City, Ben Chilwell, ambaye anaweza kumgharimu Pauni 60 milioni, kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Kai Havertz na straika wa RB Leipzig, Timo Werner.

Golini, kutokana na kipa Kepa Arrizabalaga kuwa kwenye shaka makubwa huko Stamford Bridge, Roman Burki wa Borussia Dortmund sasa anapigiwa hesabu na Lampard.