Kocha Villa amhakikishia namba Samatta Jumanne

Muktasari:

Samatta alijiunga na Aston Villa kwa dau la Pauni  10 milioni (Shilingi 30 bilioni) akitokea Genk ambayo aliifungia mabao 10 katika mashindano yote aliyoichezea msimu huu.

BENCHI  la Ufundi la Aston Villa limemhakikishia nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta nafasi ya kucheza katika mchezo wa Jumanne dhidi ya Leicester City kutokana na kiwango bora anachoonyesha mazoezini.

Kocha wa Aston Villa, Dean Smith alisema kuwa licha ya Samatta kuonekana anapata wakati mgumu kuhimili mazoezi mazito ambayo amekutana nayo katika klabu hiyo, haoni sababu ya kutompa nafasi katika mchezo dhidi ya Leicester City akiamini atakuwa chachu kwao kufanya vyema.

"Amefanya mazoezi na sisi Alhamisi na ameonyesha kiwango kizuri. Anahitajika kuendana na kasi na anafahamu kwamba kiwango cha mazoezi ni cha tofauti na alivyokuwa Genk.

"Wachezaji wengi wamekutana na kiwango tofauti cha mazoezi pindi walipokuja katika ligi  hii. Kwa hiyo mazoezi yetu ni magumu na anatakiwa azoee kwa haraka.

"Amepata utulivu na ni mchezaji mwenye haiba nzuri na itakuwa jambo jema kumjumuisha kwa namna fulani. Ni miongoni mwa walio tayari kujumuishwa Jumanne dhidi ya Leicester City," alisema Smith.