Kocha: Nilipingwa kumpeleka Simbu mbio za marathoni

Monday May 18 2020

 

By Imani Makongoro, Mwananchi imakongoro@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Alphonce Simbu akitamba nchini kwenye mbio za marathoni hivi sasa, kocha Francis John ameeleza namna alivyopingwa kumhamishia mkimbiaji huyo kwenye mbio hizo ndefu za barabarani (kilomita 42).

Francis ambaye ni kocha binafsi wa Simbu, amesema katika mahojiano na Mwananchi kuwa, hakuna aliyejua kama Simbu anaandaliwa kukimbia mbio hizo zaidi yao wawili na alipata changamoto kumuombea kibali kwenye Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ili akakimbie mbio za kufuzu mashindano ya duniani.

“Nilitaka afuzu kukimbia mbio za dunia, lakini katika marathoni huo ndiyo ulikuwa mpango wangu kwake, alipoanza kujifua ili akimbie marathoni hakuna aliyejua, changamoto ikaja kwenye kila mbio ya kimataifa tuliyoomba akakimbie walisema Simbu si mwanariadha wa marathoni,” alisema Francis.

Alisema alizungumza na wakala raia wa Uingereza ambaye ni rafiki yake akamwambia kuna mbio Australia, na wenye mbio wako tayari kulipia hoteli na Simbu ajigharamie tiketi. “Nilisema sawa watutumie mualiko, changamoto ikawa kwenye kumuombea kibali, RT walinigomea wakasema Simbu si mwanariadha wa marathoni, lakini baada ya muda wakanipa kibali akaenda Australia na kukimbia muda wa saa 2.12 (muda wa kufuzu ulikuwa saa 2.16) na akawa amefuzu kwenye mbio za dunia.”

Alisema alizungumza na Simbu ili ahamie kwenye marathoni baada ya kumpeleka kwenye mbio nchini Korea ambako alishinda medali ya fedha ya nusu marathoni.

“Simbu alikuwa akisoma Winning Sprit Sekondari, nilikuwa mwenyekiti wa bodi pale, siku moja Ezekiel Ngimba alikuwa akijiandaa kwenda kwenye mbio Korea alitakiwa mtu mwingine wa kuongozana naye ndipo akamleta Simbu kwangu,” alisema kocha huyo.

Advertisement

“Nilimuuliza Simbu uko tayari kwenda Korea, akasema niko tayari. Basi wakaanza mazoezi, katika zile mbio za nusu marathoni Simbu akamaliza wa pili na Ngimba wa nne.”

Alisema baada ya hapo Simbu hakuwa akifanya vizuri mbio za uwanjani ndipo wakakubaliana ageukie zile za marathoni na kuanza mazoezi kimya kimya.

“Baada ya mbio za Australia, tulikwenda China kwenye mashindano ya dunia, Simbu alimaliza wa 12 duniani na kuwa kwenye gredi ya kwanza ya nyota 20 waliofuzu kushiriki Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil. Simbu, amefanikiwa kufuzu kwa ajili ya mbio za Olimpiki zitakazofanyika huko Tokyo nchini Japan mwakani.

Advertisement