Kipa Shirima anatuanzishia mjadala mpya

HABARI iliyonisisimua wiki hii ni ya kipa kinda, Brian Shirima aliyepo nchini Ukraine kuelezea ndoto zake za kuchezea timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na baadaye ile ya wakubwa ‘Taifa Stars’ Kipa huyo mwenye miaka 13, hadi sasa amejipatia sifa kubwa katika mashindano ya vijana nchini humo na kuwa chagua la kwanza katika nafasi ya mlinda mlango katika timu yake ya vijana ya Oboron.

Kwa muonekano wa rangi ni mzungu lakini uraia wake ni wa Tanzania, Baba yake, Rustice Shirima ni Mtanzania anayeishi na kufanya kazi nchini Ukraine wakati mama yake ni Larysa Shirima, raia wa Ukraine.

Brian amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vijana mara tatu kuanzia mwaka 2017, 2018 na mwaka jana. Mashindano hayo yanaitwa ‘Ukrainian Children Championship’

Mbali ya mataji hayo, kipa huyo amefanikiwa pia kutwaa ubingwa wa mashindano ya Mji wa Kiev yajulikanayo kwa jina la Champions of Kiev and Kiev Region kwa miaka ya 2018 na 2019 na vilevile ameiwezesha klabu yake kutwaa ubingwa wa mashindano ya dunia ya World Trophy in Klagenfurt Austria (World Mini Trophy) mwaka 2017 na vile vile mashindano ya Ulaya ‘European Trophy in Sofia Bulgaria (Europe Mini Trophy) ya mwaka 2019.

Jambo la kwanza na la msingi ambalo tunatakiwa kufanya ni kuona fahari pindi wachezaji wa aina ya Shirima wanapoonyesha utayari wa kuchezea Taifa Stars na timu nyingine za taifa za vijana.

Hawa wanaweza kuwa na faida na mchango mkubwa kwa timu yetu ya taifa kwa sababu wamekulia katika misingi sahihi na ya kisasa ya soka ambayo imewaandaa vyema kuwa wachezaji wa daraja la juu. Wamefundishwa na wana uelewa mpana wa jinsi mchezaji anavyopaswa kuishi kiweledi ndani na nje ya uwanja ili aweze kulinda kipaji chake, lakini pia kucheza kimbinu jambo ambalo wachezaji wengi hapa nchini wanalikosa.

Tuna kundi kubwa la wachezaji ambao hwapati msingi mzuri kuanzia chini jambo ambalo limewafanya washindwe kuishi kama wachezaji wa kulipwa na wanaotambua wajibu na majukumu yao kwa timu.

Hili sio tu limekuwa likigharimu timu zetu za taifa na klabu bali pia ni miongoni mwa sababu ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikichangia kuwanyima fursa ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kulinganisha na wachezaji wa mataifa mengine.

Baada ya hilo inabidi tujadiliane mambo kadhaa ambayo yanaweza kutufanya tunufaike au tushindwe kunufaika na uwepo wa wachezaji wa asili ya Kitanzania ambao, ama wamezaliwa na kukulia Ulaya au wamekwenda huko wakiwa na umri mdogo.

Kwanza ni uwezekano wa yeye siku za usoni kubakia na uraia wa Tanzania ambao, utamuwezesha kikanuni aweze kuchezea timu zetu za taifa za vijana au ile ya wakubwa. Hili ni jambo gumu kidogo kwa sababu katiba na sheria za nchi yetu hazitoi ruhusa kwa mwananchi wake kuwa na uraia wa nchi mbili tofauti kama ilivyo kwa mataifa mengine. Hawa akina Brian na wenzao wengi hushindwa kuitumikia Tanzania kwa sababu huamua kubaki na uraia wa nchi za huko waliko kutokana na faida na fursa nyingi wanazopata.

Lakini, ikiwa uraia wa nchi mbili ungekuwa unaruhusiwa, maana yake ingekuwa rahisi kwao kuzitumikia timu zetu za taifa na kisha baada ya hapo waendelee na maisha mengine huko waliko.

Labda Shrima na wenzake wanaweza kuchukua uamuzi mgumu wa kukana uraia wa hizo nchi waliko na kuamua kubakia na ule wa Tanzania, hapo napo kuna jambo lingine linalohitaji kulitazama, je tuko tayari kuishi na wachezaji wa namna hiyo?

Kuna hulka fulani ya ubaguzi ambayo kundi kubwa la Waafrika tumekuwa nayo kwamba, wachezaji wenye ngozi nyeupe au wenye asili ya kizungu sio Waafrika au raia wenzetu katika nchi tulipo hata kama wanatimiza vigezo vyote vya kikatiba kuwa raia wa nchi husika.

Je Watanzania tutakuwa tayari kuachana na dhana hiyo pindi akina Shirima na wengineo watakapoamua kurudi kuchezea timu zetu za taifa?

Je wachezaji wetu wazawa wa hapa Tanzania watakuwa na utayari wa kifikra kuishi na kufanya kazi na wenzao ambao, hawajazaliwa au kukulia hapa nchini kama wanavyopeana ushirikiano wao kwa wao ambao, wamezaliwa na kukulia hapa nyumbani?

Ni vyema kuwa na kundi kubwa la akina Shirima kwenye timu zetu za Taifa lakini kabla ya hilo kutokea, tujadiliane jinsi ya kuishi nao.