Kina Salamba wataibuka tena mitaa ya Kariakoo

WALE Kulwa na Doto pale mitaa ya Jangwani na Msimbazi tayari wameshaanza kuteka magazeti, mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kipindi hiki ambacho Ligi Kuu inaelekea ukingoni.

Siyo kwa sababu ya vita ya ubingwa iliyopo baina yao wala siyo kwa sababu ya mabao ya kina Meddie Kagere, Heritier Makambo wala pasi za mwisho zinazopigwa na nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu.

Ni mbwembwe na tambo nyingi za usajili ambazo klabu hizo mbili zimekuwa zikihusishwa nazo kwa wachezaji kutoka klabu mbalimbali za nje na ndani ya nchi.

Kila mmoja anatamba kivyake ilimradi tu avuruge hali ya hewa upande wa pili. Mwingine anatamba kufanya usajili wa mchezaji yeyote yule anayemhitaji hata ikiwa wa mtani wake na mwingine anatamba kuwa hakuna mchezaji wake anayeweza kuhamia kwa jirani.

Ndiyo maisha tuliyoyazoea katika soka letu na inavyoonekana tutachukua muda mrefu kuachana nalo kwa sababu asilimia kubwa ya mashabiki wa soka hapa Tanzania walianza kupenda timu kabla ya mpira na ndiyo maana huwa wanapenda kusikia habari tamu tu kama hizo za usajili.

Kwa bahati mbaya mbwembwe na tambo hizi za usajili mara kwa mara zimekuwa zenye lengo la kutaka tu kujionyesha kuwa upande fulani una nguvu na jeuri ye fedha kuliko mwingine.

Usajili huu mara kwa mara umekuwa ukisababisha viongozi wa timu hizi kwenda kinyume cha matakwa na mapendekezo ya benchi la ufundi juu ya mchezaji gani asajiliwe na mchezaji gani aachwe.

Siyo jambo la kushangaza kuona benchi la ufundi likipendekeza wachezaji fulani wasajiliwe lakini viongozi wa timu husika wakashindwa kufanya usajili wa wachezaji husika kwa sababu tu wanatajwa kuwa ni mashabiki wa upande mwingine.

Lakini ni kipindi hiki ambacho mchezaji fulani anaweza kusajiliwa pasipo kufuata mapendekezo ya kocha ilimradi tu timu husika imzuie kujiunga na upande wa pili jambo ambalo limekuwa likijirudia kila msimu.

Kwa bahati mbaya usajili wa mbwembwe na kukomoana kama ambavyo umekuwa ukifanywa na timu zetu umekuwa hauna manufaa na badala yake hugeuka kuwa mzigo kwa sababu wachezaji wanaosajiliwa kwa staili hii hugeuka kuwa mzigo kwa kushindwa kufanya vizuri.

Kutofanya kwao vizuri siyo kwa sababu viwango vyao huwa chini, bali ni matokeo ya wengi wao kushindwa kuingia na kufiti kwenye mfumo wa kocha na hii ni kwa sababu usajili wao haukutokana na mapendekezo ya makocha husika.

Ni mara chache sana hutokea mchezaji ambaye husajiliwa kwa mapendekezo ya kocha kushindwa kufanya vizuri kwa sababu aliyemsajili anajua ni kwa namna gani amtumie ili aweze kuwa na manufaa kwenye kikosi chake.

Klabu zetu zinapaswa kubadilika na kuanza kuzingatia misingi ya weledi katika soka kwenye kipindi cha dirisha la usajili na kuondokana na utamaduni wa kufanya usajili wa mashindano na mbwembwe ambao hatimaye umekuwa hauzisaidii na badala yake kugeuka kuwa shubiri.

Usajili unapaswa kuendana na mahitaji ya benchi la ufundi ambalo ndilo linajua litatumia vipi wachezaji waliopo kikosini ili kuweza kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.

Viongozi wanapaswa kusikiliza na kufanyia kazi kile ambacho benchi la ufundi litapendekeza lakini pia na wachezaji nao wanapaswa kuwa makini na kuepuka tamaa ambazo zitasababisha kuathiri viwango vyao kwa kukimbilia timu fulani.

Nyota wetu wanapaswa kuwaza zaidi fursa za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi badala ya kutamani kuingia kwenye mkumbo wa usajili wa mbwembwe ambao umekuwa ukifanywa na klabu zetu hasa Simba na Yanga.

Klabu zetu ziachane na usajili wa kutafuta sifa na badala yake zisajili wachezaji sahihi ambao wanatokana na mapendekezo sahihi ya benchi la ufundi.

Ni vigumu kuamini kuna kocha anayeweza kupendekeza usajili wa mchezaji wa nafasi fulani ambayo tayari ina wachezaji zaidi ya watatu ambao wanaonekana wana viwango bora zaidi ya huyo aliyesajiliwa.

Ilitokea kwa Simba ilipoamua kumsajili Adam Salamba kutoka Lipuli wakati huo kikosini ikiwa na Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza ambao walikuwa wanaonyesha viwango bora.

Ilionekana wazi ulikuwa ni usajili wa kuikomoa Yanga ambayo nayo ilimtaka kinda huyo wa Lipuli na siyo mapendekezo ya benchi la ufundi ambalo kwa sasa limekuwa likimuweka benchi.

Badala ya kujifunza kutokana na makosa, tunaweza kushuhudia usajili wa namna hiyo kwa mara nyingine tena.