Kiiza aishangaa Yanga kumtema Balinya

Muktasari:

Balinya alisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili mwanzoni ma msimu huu na kushindwa kuonyesha uwezo uliokuwa unatarajiwa na wengi na dirisha dogo la usajili akavunjiwa mkataba wake na kuamua kurudi kwao Uganda na baadaye kujiunga na Gor Mahiya ya Kenya.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba na Yanga, Hamis Kiiza amewatolea uvivu viongozi wa Yanga kuwa walikurupuka kufanya maamuzi ya kuachana na Juma Balinya na kuweka wazi kuwa walitakiwa kumpa muda zaidi.

Balinya aliachana na Yanga dirisha dogo la usajili baada ya kushindwa kuendana na kasi ya timu hiyo na sasa anakipiga Gor Mahiya inayoshiriki Ligi Kuu Kenya ambapo hadi sasa ameifungia mabao mawili.

Kiiza alisema ligi ya Tanzania ni ngumu inahitaji mchezaji kupewa muda ili kuzoea na kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa mwalimu na kuonyesha kile alichonacho mguuni.

"Nalifahamu vizuri soka la huko na nimecheza kwenye timu zote mbili zenye mashabiki wengi viongozi hawana uvumilivu kinachonishangaza kwa upande wa Yanga ni kumuacha Balinya ambaye kwa usajili walioufanya hasa safu ya ushambuliaji huyo ndiye aliyekuwa na rekodi nzuri alikotoka,"

"Wanamuacha mchezaji ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi Uganda na kumuacha mshambuliaji ambaye alikuwa amekaa nje kwa muda kwa kigezo cha kufunga mabao akiwa anapewa nafasi huku Balinya akiachwa benchi," alisema.

Kiiza aliongeza kuwa anampongeza Balinya kwa kutokata tamaa na kuamini katika uwezo kwa kusaini timu nyingine na kuanza kwa kishindo huku akiamini kuwa atafanya mambo makubwa ambayo yatawafanya viongozi wa Yanga wajilaumu.