Kessy awashangaza Wazambia

Friday September 14 2018

 

By OLIPA ASSA

HASSAN Kessy aliyekuwa akiichezea Yanga amewashangaza Wazambia kwa kutua Nkana FC na kuingia kikosi cha kwanza, lakini mwenyewe amefichua alijiongeza mapema mara alipotua katika klabu hiyo ya Ligi Kuu.

Kessy alikiri kwamba Ligi ya Zambia ni tofauti na ilivyo Ligi Kuu Bara kutokana na matumizi ya nguvu na wachezzxaji kutochoka kwa dakika 90, ila alisema alibaini hilo alipotambulishwa na kuishuhudia Nkana ikicheza kwa mara ya kwanza na kuwaduwaza nyota aliowakuta kikosini, ikizingatia anatokea Tanzania.

“Nilipofika nilianza kuwasoma wachezaji kwanza ni wa aina gani ndipo nikajua jamaa ni watu hatari soka kwao ni kazi kweli kweli, mazoezi wanaanza kabla ya kocha na akiwakuta wanaendelea kwa kasi ile ile,” alisema na kuongeza.

“Nilibaini lipo jambo kocha analitegemea kutoka kwangu na nilipotambua nilifanya juhudi, nikajiamini, nikazingatia nidhamu na nikajituma kwa bidii, uzuri niliyapenda mazoezi tangu nacheza Tanzania na ndio nimeingia kikosini haraka.”

Alisema kwa aina ya mazoezi na maandalizi ya timu za Zambia ndio maana imefanya wachezaji wake wawe na stamina, wasiochoka na wanaojituma uwanjani kwa dakika zote bila kuchoka.

“Ndio sababu ligi yao ni ngumu na hata wachezaji wanaokaa benchi sio wa ovyo ni watu wenye uwezo wao, ila ni kwa kuwa mechi lazima timu ianze na wachezaji 11,” alisema Kessy ambaye hajutii kutimka Yanga.

“Nina mtazamo wa kufika mbali, ili timu ya taifa yaani Taifa Stars iwe bora wachezaji tunalazimika kutoka kwenda kujifunza mbinu za kupambana kimataifa.

Hivyo siwezi kurudi nyuma napaswa kuangalia mbali pia nawashauri wachezaji wenzangu wakipata nafasi nje wasichezee kwa faida la taifa letu,” alisema Kessy.

Beki huyo wa zamani wa Simba, alisema ndani ya Nkana kuna ushindani mkubwa na anaamini inamfanya kiwango chake kizidi kuwa bora.

Advertisement