Kessy akiona cha moto Zambia

Monday February 18 2019

 

KIPIGO cha kwanza kwa Nkana Red Devils msimu huu wa 2018/19, kimekingiwa kufua na beki wa Kitanzania anayeichezea klabu huyo, Hassan Kessy kwa kisingizio cha kuwa Ligi Kuu Zambia bado mbichi sana.

Nkana wamekiona cha moto ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kwa kutandikwa mabao 2-0 na Power Dynamos.

Kessy alisema wamejikwaa kama timu na sio mchezaji mmoja mmoja kilichopo ni kusimama na kuangalia yaliyopo mbele yao kutokana na malengo mazito waliyonayo msimu huu.

“Msimu huu tumepanga kuchukua ubingwa wa ligi, kupoteza mchezo mmoja haina maana kuwa kasi yetu itapungua. Ni vigumu kumaliza msimu bila ya kupoteza kutokana na ushindani uliopo.

“Inshu ya rekodi sijui kumaliza msimu bila ya kupoteza sio kitu kibaya ila hilo halipo kwenye vipaumbele vyetu pamoja ya kuwa kila tunapojiandaa tumekuwa tukitaka kushinda,” alisema.

Mchezo huo ambao Nkana imepoteza ni wa mzunguko wa nne, katika mechi nyingine imeshinda moja mbele ya NAPSA Stars na imetoka sare mara mbili dhidi ya Forest Rangers na Lumwana Radiants.

Msimu uliopita ambao Nkana ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya ZESCO United F.C na ilipoteza michezo sita.

Advertisement