Kesi ya Yanga ipo palepale

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), Ally Mchungahela

YANGA mmesikia huko? Juzi mabosi wa Yanga wametangaza mchakato wa uchaguzi wao kuanza upya, lakini wanachama waliofungua kesi kupinga matumizi ya kadi za Posta katika uchaguzi huo bado wameshikilia msimamo wao.

Wanachama hao walisema kesi hiyo bado ipo pale pale hadi uchaguzi wa klabu hiyo utakapofanyika.

Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13, 2019, lakini ulisimamishwa baada ya wanachama wawili kufungua kesi ya kikatiba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mmoja wa wanachama waliofungua kesi hiyo, Juma Magoma alisema hawawezi kufuta kesi hiyo kwa sababu wanasimamia katiba ya klabu yao. “Tunachokisubiri sisi ni tarehe ya uchaguzi itangazwe na TFF ambao wamepewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi huo baada ya viongozi wa Yanga kusuasua kufanya uchaguzi huo.

“Hatuna taarifa juu ya uchaguzi huo kufutwa na kuanza upya kwa mchakato kwa sababu Serikali iliyokuwa imepewa mamlaka ya kuusimamia haijatoa taarifa hivyo tunachokisubiri ni tarehe.

Alihoji; “Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, George Mkuchika ni nani hadi aufute uchaguzi uliopangwa kufanyika kwa mujibu wa serikali na hata ukifutwa tunasubiri taarifa itoke serikalini kama walivyofanya walivyokuwa wanatangaza kuusimamia uchaguzi huo.”

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), Ally Mchungahela alipotakiwa kufafanua juu ya hilo alijibu kwa ufupi; “Nitalitolea ufafanuzi hivi karibuni, tuwe wavumilivu.”