Kapombe afichua siri Stars

Muktasari:

  • Kapombe alionyesha utofauti mkubwa katika uchezaji wake na jinsi ambavyo alicheza Hassan Kessy katika mchezo uliopita.

BEKI wa Simba na Taifa Stars, Shomari Kapombe katika mchezo dhidi ya Cape Verde alionyesha umahiri mkubwa wa kupandisha mashambulizi akitokea upande wa kulia na kugeuka mwiba katika safu ya ulinzi ya Cape Verde.

Uchezaji wake ulikuwa tofauti na Hassan Kessy ambaye alicheza mchezo wa kwanza huku mchezo huu akikosekana kutokana na kadi mbili za njano alizozipata mechi zilizopita dhidi ya Uganda na Cape Verde.

Katika mchezo wa kwanza washambuliaji wa Cape Verde walikuwa wakitumia upande wa Kessy kupenyeza mashambulizi, lakini mchezo huu hali ilikuwa tofauti kwani walikwama kabisa mbele ya Kapombe.

Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mechi hiyo kumalizika ambapo Stars ilishinda bao 2-0 uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Kapombe alisema mbinu hiyo alipewa na kocha baada ya kupitia mechi iliyopita namna ambavyo walikuwa wakicheza wapinzani wao.

“Mwalimu aliniambia nihakikishe napeleka mashambulizi kwa haraka mno kwa sababu wenzetu walikuwa wanaingiza winga mmoja ndani, hivyo nitumie nafasi hiyo kupiga krosi, vile vile kurudi kuzuia haraka pale ninapoacha nafasi, nashukuru nilifanikiwa kufanya kile nilichoelekezwa kukifanya,” alisema.

Kapombe aliongeza kwamba bado wana imani ya kufanya vizuri mchezo ujao kutokana na kocha wao Emmanuel Amunike kuwa mtu wa kufuatilia wapinzani mapema kabla hawajakutana nao katika mchezo mwingine.