Kane apiga hesabu za Ligi ya Mabingwa

LONDON ENGLAND. STRAIKA, Harry Kane amesema timu yake ya Tottenham Hotspur inahitaji kushinda mechi nane kati ya tisa walizobakiza kwenye Ligi Kuu England ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Spurs wapo kwenye nafasi ya nane katika msimamo, pointi saba nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, Chelsea — lakini baada ya janga la corona kupita na ligi kutarajia kurudi upya, wanaamini watapambana kufanikisha hilo.

Straika Kane, Son Heung-min na Steven Bergwijn — wote walipata majeraha ambayo yalitishia uwezekano wao wa kucheza tena msimu huu, sambamba na Moussa Sissoko, lakini baada ya ligi kusimama kutokana na janga la corona kwa zaidi ya miezi miwili, wakali hao sasa wapo fiti kwa ajili ya kuipambania timu yao.

Kane alisema: “Tunapaswa kumalizia kwenye Top Four, hakuna ubishi wa hilo. Tuna mechi ngumu dhidi ya Manchester United, lakini ukweli ni kwamba tunahitaji kushinda mechi saba au nane ili kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.”

Ufiti wa Kane utakuwa muhimu zaidi kwa Spurs, baada ya kupata majeraha ya misuli yaliyomfanya awe nje ya uwanja tangu siku ya Mwaka Mpya. Lakini, kwa sasa yupo vizuri na alisema: “Ilikuwa jambo zuri kupata yale mapumziko.

“Sijacheza mechi kwa miezi sita sasa, ni muda mrefu sana. Kuhusu kuwa majeruhi, sasa hivi nipo fiti.

“Najisikia vizuri, najisikia nina makali. Nimekuwa nikifanya mazoezi sana binafsi na kuboresha kiwango changu.”

Straika kinda wa Spurs, Troy Parrott, 18, atakosa mwendelezo wa ligi itakapoanza baada ya kufanyiwa upasuaji wa kidole tumbo.

Kane amefunga mabao 11 na kutoa asisti zilizozaa mabao mawili katika mechi 20 za Ligi Kuu ya England alizocheza msimu huu ambao amekuwa akisumbuliwa na majeraha..