Kane apewa bao la mezani kumfukuzia Mo Salah

Muktasari:

  • Mwanzoni bao hilo alipewa Christian Eriksen, akidhaniwa ndiye aliyefunga, lakini Kane amekuwa akilalamika kunyimwa bao hilo kwa sababu mpira ulimgonga kwenye bega kabla ya kutinga wavuni.

LONDONENGLAND


UMESIKIA huko? Harry Kane amelilia bao la Stoke City hadi amelipata na hakika jambo hilo halikumfurahisha supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah katika mbio za kufukuzia Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England msimu huu.

Mwanzoni bao hilo alipewa Christian Eriksen, akidhaniwa ndiye aliyefunga, lakini Kane amekuwa akilalamika kunyimwa bao hilo kwa sababu mpira ulimgonga kwenye bega kabla ya kutinga wavuni.

Na sasa taarifa ya Ligi Kuu England ilitoa taarifa yake iliyosomeka: “Harry Kane amepewa lile bao la pili la Tottenham Hotspur dhidi ya Stoke City kwenye ushindi wao wa 2-1 Jumamosi iliyopita baada ya klabu na mchezaji kukataa rufaa Kamati ya Utambuzi wa Mabao ya Ligi Kuu England.

“Bao hilo mwanzoni alipewa Eriksen kwenye siku ile ya mechi, lakini baada ya taarifa za mchezaji na kutazamwa upya kwa picha za video, kamati ya watu watatu ilikubaliana mpira ulimgusa Kane kabla ya kutinga wavuni, hivyo bao hilo ni lake. Kane sasa atakuwa na mabao 25 Ligi Kuu England msimu huu wa 2017/18.”

Jambo hilo limemshtua Salah na kuamua kutumia ukurasa wake wa Twitter kuandika ujumbe huu: “Woooooow really?” akionekana kushangazwa na uamuzi huo. Fowadi huyo wa Liverpool amefunga mabao 29 kwenye Ligi Kuu England na ndiye kinara wa mabao. Mastaa kibao wa Liverpool na wanasoka wengine walionekana kubonyeza kitufe cha ‘like’ kuhusiana na komenti hiyo ya Salah kwenye Twitter.

Kane, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu England kwa misimu miwili iliyopita, anataka shinda tena huku Salah akionekana kumkosesha raha na hivyo kumfanya alazimishe kupata mabao mengine ambayo inahitaji kutazama video zaidi ya mara moja.