Kanda ya Ziwa kazi ipo

Tuesday January 8 2019

 

By Saddam Sadick

MWANZA.UKUBWA wa kichwa sio wingi wa akili, Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mambo kutoenda sawa kwa timu za Kanda ya Ziwa wakati duru la pili likianza kuashiria ngwe ya lala salama ya Ligi Kuu Bara.

Msimu wa 2018/19 Kanda ya Ziwa imepata neema kubwa ya kuwakilishwa na timu sita katika ligi hiyo, lakini kutokana na matokeo yake bado hayajaridhisha na huenda duru la pili kama hazitashtuka itabaki historia tu.

Hadi kumalizika kwa mechi zao za raundi ya kwanza ni timu tatu tu zilizopo katika nafasi nzuri kwenye 10 Bora ambapo Mbao ipo nafasi ya tano na alama zao 27, kisha Kagera Sugar yenye pointi nafasi ya nane na Mwadui waliopo nafasi ya 10 na alama 24.

Kwa matokeo hayo, timu hizo zitapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha zinasalia kwa msimu ujao vinginevyo kuna baadhi zitaenda maji na kuacha historia ya ushiriki.

Mwanaspoti imeangalia mwenendo wa timu zote za Kanda ya Ziwa ikiwamo usajili na mabadiliko katika benchi la ufundi na kukuletea uchambuzi wa kina kwa timu moja moja ambao unaweza kuzibeba au kuzishusha daraja.

MBAO FC

Timu hii ya Jijini Mwanza ina msimu wa tatu kushiriki Ligi Kuu, imekuwa na mwanzo mzuri wa ligi hiyo na sasa ndio klabu inayoongoza kwa Kanda ya Ziwa, huku ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo.

Licha ya nafasi hiyo nzuri waliyonayo, bado haiwezi kutamba eti imeshajihakikishia kubaki Ligi Kuu, kwani ikijichanganya tu inaweza kuzisahau Simba na Yanga na kuacha historia.

Mbao hivi karibuni iliachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Amri Said ‘Jaap Stam’ na kuikabidhi timu kwa Msaidizi wake, Ali Bushiri ‘Benitez’ kutokana na kulingana kiwango cha elimu (leseni B).

Kuondoka kwa Stam aliyeiacha Mbao katika nafasi ya nne kwa pointi 24, inaweza kuwa sababu ya kushuka kwao, kwani hadi sasa tayari imeshuka nafasi mbili hadi kufikia nafasi ya sita.

Pia inawezekana kuwa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wameshamzoea Kocha huyo inaweza kuwapa wakati mgumu kumuelewa kocha mpya na kusababisha kutoelewana na mwisho kupata matokeo mabovu na kujikuta wakishuka daraja.

Lakini pia kuja kwa Benitez kunaweza kukaisaidia Mbao kupata matokeo mazuri kutokana na mbinu mpya alizokuja nazo kikosini ambazo wachezaji wanaweza kuzitumia katika mzunguko wa pili na kupata matokeo mazuri.

Kuhusu usajili Mbao imesajili pengine kadri ya mahitaji ya timu,hivyo ni uongozi kuhakikisha unaweka mipango thabiti na rafiki kwa wachezaji na benchi la Ufundi kuweza kufikia malengo yao,huku mashabiki na wadau wa soka Jijini kutoa sapoti.

KAGERA SUGAR

Chini ya Mecky Maxime matokeo yake bado ni ya kawaida na kama haitakaza lolote linaweza kuikuta kwani nafasi na ponti walizonazo kwenye Ligi si rafiki sana na inahitaji juhudi binafsi. Kagera yenyewe haijafanya mabadiliko yoyote kuanzia dirisha dogo la usajili hadi kwenye benchi la ufundi, mwenendo wake upo wastani na ikumbukwe mwanzoni ilipata tabu katika kusaka pointi tatu.

Wenyeji hao wa Bukoba matokeo yake asilimia kubwa ni sare, hivyo kama duru la pili haitapambana kuhakikisha kila mchezo inavuna pointi tatu inaweza kujikuta katika Ligi Daraja la kwanza.

Kiushindani Kagera imepambana licha ya kwamba timu kubwa ilizocheza nazo ikiwa ni Azam na Yanga ilipoteza, lakini nayo iliweza kujidhatiti vyema kuzichapa timu ndogo ndogo na nyingine ikitoka nazo sare.

STAND UNITED

Chama la Wana kutoka Shinyanga hali yake haijatulia na kama itajichanganya inaweza kuondoka na maji, mabadiliko yaliyofanyika haswa kwenye usajili yanaweza yasiiache salama kama haitakuwa makini.

Hadi sasa Kocha Mkuu, Amars Niyongabo haijaeleweka kama bado anaendelea kuinoa au ndio basi tena, kwani tangu mapumziko mafupi ya kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) bado hajaungana na timu. Pia Stand imeondokewa na nyota wake wengi waliokuwa na uwezo na uzoefu wa Ligi Kuu na kuamua kuwasajili wachezaji chipukizi hivyo mabadiliko hayo yanaweza kuwa na mambo mawili.

Bigirimana Blaise, Adventure Pastory, Erick Mlilo, Mussa Kilingi, Sixtus Sabilo na Juma Ally wamesepa na kuwasajili chipukizi kutoka timu za madaraja ya chini, jambo ambalo linaweza kuwabeba au kuwashusha.

MWADUI FC

Licha ya soka safi na la ushindani kwa timu hii ya Shinyanga, ila nayo inapumulia mashine japo duru la pili imeanza kwa mkwara kwa kuifanyizia Kagera Sugar ikiipa kipigo kikali zaidi msimu huu cha mabao 4-0.

Hadi sasa ipo nafasi ya 10 kwa pointi 24 ambapo isipozichanga vyema karata zake katika ngwe hii ya mwisho inaweza kujutia zaidi, hivyo Kocha Ally Bizimungu anahitaji kufanya mapinduzi ya kweli kuinusuru timu hiyo.

Pia klabu hii haijafanya mabadiliko makubwa katika dirisha dogo la usajili ikiwa ilimuongeza kikosini Straika Ditram Nchimbi kutoka Azam kwa mkopo, ambaye amefika na kutupia mabao mawili wakati wakiishindilia Ndanda mabao 3-0.

Puia amekuwa akisaidia sana timu kutengeneza mabao, ikiwemo alivyofanya juzi dhidi ya Kagera na kusaidia Mwadui kupata ushindi wa pili mfululizo nyumbani.

ALLIANCE FC

Hawa ni wageni wa Ligi Kuu hakuna asiyekumbuka changamoto iliyoanza nayo kwa kuchezea vichapo na kutabiriwa mapema kushuka Daraja kutokana na matokeo ambayo iliyapata ya kusikitisha.

Alliance ilifikia hatua ya kujikuta ikiachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wake, Mbwana Makata aliyedai alikuwa akiingiliwa majukumu, lakini hata hivyo matokeo yake hayakuwa sawa.

Licha ya sasa kuonekana kubadilika na kujinasua mkiani chini ya Kocha mpya, Malale Hamsini lakini bado ina hali ngumu kama haitaweza kupambana mechi raundi ya pili na kujikuta ikirudi Daraja la Kwanza.

Ni kama ilishtuka kwa jinsi ilivyofanya usajili ambao umeanza kuonyesha picha nzuri kwani ujio wa mastraika Hussein Javu na Bigirimana Braise na kipa John Mwanda umeongeza kitu kipya ndani ya timu hiyo. Tumeshuhudia kuja kwa washambuliaji hao, tayari wameshacheka na nyavu.

BIASHARA UNITED

Klabu hii ina hali mbaya kweli kweli na wiki iliyopita ikiongozwa na Kocha mpya, Amri Said ‘Stam’ iliweza kuonja ushindi ikiwa uwanja wa nyumbani kwa kuichapa Mbeya City na kufufua kidogo matumaini.

Timu hii iliyokuwa chini ya Kocha Mnyarwanda Hitimana Thiery ilikuwa na matokeo mabaya kiasi kwamba ilicheza mechi 17 na kubaki mkiani kwa pointi 10 na kusababisha uongozi kufikia hatua ya kuachana na Mnyarwanda huyo.

Kwa sasa Stam ameiongoza mechi mbili na kuvuna pointi nne ikiwamo moja ya suluhu waliopata dhidi ya Singida United, japo bado ana kazi ya kuiongoza timu hiyo ya Mara ili isishuke daraja.

Advertisement