Kambi yampa mzuka Aussems

Muktasari:

Akizungumza na Waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini, alisema kambi imekwenda vizuri licha ya kukutana na changamoto ndogondogo.

KOCHA wa Simba, Patrick Aussems amesema kambi ya wiki mbili ambayo waliweka nchini imemsaidia kuweza kujenga utimamu wa mwili kwa wachezaji wake.


Akizungumza na Waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini, alisema kambi imekwenda vizuri licha ya kukutana na changamoto ndogondogo kulingana na mazingira ya ugenini.


"Jambo kubwa ambalo nashukuru ni kwamba lengo kubwa katika maandalizi ya msimu ujao yalikuwa ni utimamu wa mwili, nashukuru jambo hilo tumeweza kwa kiasi kikubwa kulitengeneza kwa asilimia nyingi," alisema.


Akizungumzia kwa upande wa wachezaji wake walio ondoka na kurejea nchini kwajili ya kujiunga na kambi ya timu ya Taifa Tanzania, alisema jambo hilo lilivuruga mipango yake.


"Kama ambavyo unajua kwamba wachezaji wetu walirudi huku, kiukweli walivuruga mipango yangu hasa ya kimbinu, lakini hilo halitosumbua kwa sababu hawa ni wachezaji wetu na wanajua wapi tulipoishia," alisema.


Aliongeza michezo ya kirafiki waliyocheza imewasaidia kwa namna moja ama nyingine kuweza kuona mapungufu ya kikosi pamoja na ubora wa kila mchezaji
"Tumecheza na timu bora katika mechi zetu za kirafiki, ni kipimo kizuri sana kwetu kwa ajili ya kujiandaa na ligi pamoja na mashindano ya kimataifa," alisema Aussems aliyeifikisha Simba hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.