Kai Havertz atoa masharti yake

Saturday June 27 2020
kai pic

LONDON, ENGLAND. Manchester United na Chelsea wapambane tu na hali zao. Staa wa Bayer Leverkusen, Kai Havertz ameripotiwa atazipiga chini ofa zote za kutoka kwenye klabu hizo mbili za Ligi Kuu England kama hazitakuwa zimefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Havertz, anataka kucheza kwenye michuano ya Ulaya msimu ujao, hivyo jambo hilo ni mtego kwa timu za Chelsea na Man United zinazomsaka, kuhakikisha zinafanya kweli na kukamatia tiketi hiyo.

Kwa sasa, timu hizo zipo kwenye nafasi ya nne na tano, Chelsea wakiwa juu kwa tofauti ya pointi tano, huku zikiwa zimebaki mechi saba Ligi Kuu England kufika tamati.

Kama timu zote zitafuzu kucheza michuano hiyo ya Ulaya msimu ujao, basi itakuwa kazi ya Havertz kuchagua kwenda Old Trafford au Stamford Bridge.

Havertz amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akifunga mabao 16 na kuasisti mara tisa katika mechi 41 za michuano yote alizoitumikia Leverkusen.

Klabu kadhaa zimevutiwa na huduma yake zikiwamo Real Madrid na Bayern Munich pia na zimeonyesha dhamira ya kuhitaji kumsajili wakati dirisha la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Advertisement

Hata hivyo, Bild linaripoti Havertz anachokitaka ni kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo hataketi kitako kusikiliza ofa ya timu ambayo itakuwa haina tiketi ya kushiriki michuano hiyo.

Nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu England msimu huu inaweza kutoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, kama Manchester City watamaliza msimu ndani ya Top Four na hawatakuwa wameshinda rufani yao ya kupinga kufungiwa misimu miwili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Advertisement