Kagere apishana na mkwanja wa maana, meneja afunguka

Muktasari:

Licha ya Mshambuliaji Meddie Kagere kuwekewa mezani ofa ya Sh.400 mil, meneja wa mchezaji huyo Patrick Gakumba, amefikia maamuzi ya kumbakiza mteja wake katika kikosi cha Simba.

LICHA ya kwamba mshambuliaji Meddie Kagere kuhitajika na klabu tatu barani Afrika, meneja wa mchezaji huyo Patrick Gakumba, amefunguka kwamba hana mpango wa kuona mchezaji wake akiondoka hivi sasa katika kikosi cha Simba licha ya kuwekewa mezani ofa ya Dola za Kimarekani 200,000 (Sh.460 mil).

Kagere ambaye amejiunga na Simba msimu huu akitokea katika kikosi cha Gor Mahia ya Kenya amekuwa katika kiwango kizuri huku akiifungia klabu hiyo magoli 7, mpaka hivi sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gakumba alikiri kupokea ofa kutoka katika klabu tatu kubwa barani Afrika lakini alipofanya mawasiliano na Uongozi wa Simba ameona bora aendelee kumuwacha mchezaji huyo kikosini hapo.

“Nilipokea ofa kutoka Klabu za Zamalek (Misri), Premier Da Ghost na Vital Club (zote Angola) na waliweka ofa nzuri lakini Uongozi wa Simba ukaniomba mchezaji wangu aendelee kusalia na nikaona bora tu iwe hivyo,” alisema Gakumba.

Gakumba alifunguka zaidi na kusema kwamba katika maongezi yao, viongozi hao walimwambia kwamba wanataka kuifanya Simba kuwa moja ya klabu kubwa Afrika.

“Nimeiona Simba inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na  maongezi yangu na kiongozi mmoja ambaye nilimpelekea ofa ya Kagere aliniambia kwamba anatambua umuhimu wa mchezaji wangu katika kikosi hivyo dili hilo kwa sasa tulipotezee kutoka na kwamba wapo katika mashindano muhimu.” Alisema.

Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu kwamba Simba haiwezi kukubali kumwachia Kagere huku mshambuliaji wao Emmanuel Okwi naye akiwa katika rada za kujiunga na Kaizer Chiefs ambayo imeonyesha nia ya kutaka huduma yake.