Kagere: Eti Ninja? Kamuulizeni Bailly!

Friday September 14 2018

 

By THOMAS NG’ITU

MABEKI wa timu pinzani nchini wajipange kwelikweli kwa straika wa Simba, Meddie Kagere aliyerejea nchini akitokea Rwanda kuitumikia timu yake ya taifa, huku akiwa na mzuka mkubwa uliokolezwa na nyota wa Manchester United.

Ndio, katika mechi yao ya kuwania fainali za Afcon 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon, Rwanda ilivaana na Ivory Coast na kulala nyumbani mabao 2-1, huku bao la kufutia machozi likiwekwa kimiani na Kagere.

Hata hivyo, ishu sio bao lake, bali ni jinsi straika huyo alivyowapa shughuli pevu na kuizidi akili ngome ya Ivory Coast iliyokuwa ikilindwa na beki wa Man United, Eric Bailly pamoja na Serge Aurier anayekipiga klabu ya Tottenham Hotspur na Kagere amesisitiza anapokuwa kazini huwa haangalii sura ya mtu.

Akizungumza na Mwanaspoti juzi jioni mara baada ya mazoezi jijini Dar kabla ya kusafiri na timu asubuhi ya jana Ijumaa kwenda Mtwara, Kagere alisema kazi yake ni kufunga na mabeki timu pinzani wasipojipanga watapata tabu sana.

Kagere ni kama anatuma salamu mapema kwa m abeki wa Yanga wakiongozwa na Kelvin Yondani, Shaibu Abdallah ‘Ninja’, Andrew Vincent ‘Dante’ na wengine anaotarajia kukutanao nao Septemba 30 katika mechi ya Watani wa Jadi.

Nyota huyo aliyesajiliwa Simba kutoka Gor Mahia na kuichezea Simba jumla ya mechi 13 na kufunga mabao tisa mpaka sasa kwa mechi zote, alisema kitendo cha kuwaburuza mabeki wanaotamba Ligi Kuu ya England na wengine wanaocheza Ulaya, kumemfanya ajihisi ameimarika zaidi.

Alisema kwa hali hiyo haoni wa kumsumbua kwa mabeki wa timu za Ligi Kuu Bara, japo hawadharau, lakini anaamini wakifanya uzembe mbele yake ataendelea kuwaliza kama alivyofanywa kwa mabeki wa Prisons na Mbeya City.

Timu hizo mbili zilitunguliwa na Mnyarwanda huyo mwenye asili ya Uganda katika mechi mbili za awali ilizocheza Simba na kumfanye awe kinara wa mabao kwa sasa na kesho Jumamosi timu yao itawakabili Ndanda mjini Mtwara.

Kagere alitoa majibu hayo baada ya kuulizwa anamzungumziaje Eric Bailly aliyemsumbua kwenye pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Amahoro, Kigali na yeye kutupia bao la kufutia machozi kwa kichwa.

“Bailly ni mchezaji mzuri, ila nikiri kuna tofauti kubwa ya kukucheza dhidi ya mchezaji anayecheza Afrika na Ulaya, ila sio mara yangu ya kwanza kukutana na nyota kama hawa, lakini huwa najua namna ya kutekeleza majukumu yangu.”

“Naweza kusema kukutana naye kumeniongezea ufundi mwingine katika mbinu za kupenya safu za ulinzi katika Ligi Kuu na mabeki pinzani wajipange kweli, nitaendelea kufunga kama wakifanya uzembe,” alisema Kagere.

Kagere, alisema kama ya kukutana na nyota hao wa Ivory Coast alishavaana na kina Gervinho, Yaya Toure na wakali wengine, kitu kinachomfanya apate uzoefu zaidi wa kusumbua mabeki na wachezaji wa timu pinzani akutanapo nao.

Kuhusu mchezo wa kesho alisema amesikia Uwanja wa Nangwanda Sijaona una changamoto, lakini alisema atahakikisha anaendeleza rekodi yake ya kufunga kama mechi zilizopita.

“Katika maisha napenda changamoto, hivyo kama uwanja ni mbaya inabidi nitafute njia ya kunifanya nifanye vizuri mno, ukishaiweza changamoto basi umekamilika na ndivyo maisha yalivyo,” alisema.

Simba na Ndanda zinakutana kesho katika mechi yao ya tisa tangu msimu wa 2014-2015, huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa na rekodi ya kushinda mfululizo.

Advertisement