Kabwili aibukia Mwanza

Muktasari:

Yanga walioingia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba Jijini hapa, wanaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa kesho wa kirafiki dhidi ya Pamba FC .

MLINDA mlango wa Yanga , Ramadhan Kabwili aliyekuwa na timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 , leo Ijumaa amejiunga timu yake katika mazoezi ya mwisho ya timu hiyo kabla ya kukabiliana na Pamba FC hapo kesho Jumamosi.
Kabwili alikuwa kwenye kambo ya timu hiyo ya vijana inayojiandaa na mashindano ya CECAFA yanayotarajia kufanyika mwezi huu Septemba nchini Kenya.
Yanga wameweka kambi yao jijini hapa ambapo kesho watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba na Septemba 10 watacheza na Toto African kabla ya kurudi Dar es Salaam kucheza mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia, Septemba 14.
Imeelezwa kwmaba kipa huyo alijiunga na wenzake jana Alhamisi jioni ambapo katika mechi hiyo ya kirafiki ndiye atakayesimama langoni kwani makipa Metacha Mnata na Farouk Shikalo wapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa.
Katika mazoezi ya leo jioni, kocha wa makipa wa Yanga, Peter Manyika ameonekana akimfundisha kipa huyo na kumpa mbinu mbalimbali za kiufundi ikiwemo kudaka mashuti ya mbali yenye nguvu.