Kabunda ala kiapo KMC

Muktasari:

Msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara takuwa msimu wa pili kwa Kabunda kuichezea timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC)  tangu alipojikombe shirikisho,kusaini mkatabanga nayo akitokea Mwadui ya Shinyanga.

BAADA ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili na KMC, Hassan Kabunda amesema lengo lake ni kuhakikisha anaisaidia klabu yake kufanya vizuri msimu ujao wa Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya kimataifa ambapo timu hiyo imepata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Nyota huyo ambaye amekuwa akicheza kama winga na muda mwingine kiungo, alisema atashirikiana na wachezaji wenzake ili kufanikisha malengo ya klabu hiyo yenye maskani yake  Kinondoni  jijini  Dar es Salaam.
"Nimeamua kuongeza mkataba ili niendelee kuitumikia KMC, tulifanya vizuri msimu uliopita kumaliza nafasi nne za juu, msimu ujao kwa kushirikiana na wenzangu tunatakiwa kufanya zaidi," anasema Kabunda.
Kabunda ni mtoto wa beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Salum Kabunda ‘Ninja’ (sasa marehemu) aliyewika Yanga aliibukia kituo cha kukuza vipaji Dar es Salaam (DYOC) kabla ya kuchezea timu ya vijana ya Ashanti United, ambako alipandishwa hadi timu ya wakubwa na kuanzia huko kucheza Ligi Kuu.
Baada ya Ashanti kuteremka daraja, Kabunda ambaye mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu ulikuwa dhidi ya JKT Ruvu, sasa JKT Tanzania akifunga bao zuri lililompatia umaarufu, alienda kujiunga na Mwadui ambayo aliachana nayo na kuamua kurejea Dar es Salaam.
Kabunda alivyojiunga na KMC alikuwa  mchezaji mpya wa tano kusajiliwa KMC baada ya kipa Juma Kaseja kutoka Kagera Sugar na mabeki Aaron Lulambo, Ali Ali wote kutoka Stand United, Sadallah Lipangile kutoka Mbao FC na kiungo mshambuliaji, Abdul Hillary Hassan kutoka Tusker FC ya Kenya.