KMC yaipeleka Simba nafasi ya tano.

MCHEZO wa raundi ya tisa Ligi kuu bara kati ya Gwambina FC na KMC umemalizika kwa KMC kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote mbili kucheza kwa kujilinda zaidi huku wakishambuliana kwa kushitukiza katika nyakati tofauti tofauti.

Dakika ya 43 beki wa kati wa KMC Lusajo Mwaikenda aliipatia bao la kuongoza timu yake baada ya  kumalizia kwa kichwa krosi iliyopigwa na Patrick Israel  iliyotokana na mpira wa kutenga.

Kipindi cha pili kilianza kwa Gwambina kuonekana wakishambulia kwa kasi licha ya kukosa bao mpaka pale dakika ya 84, Reliant Lusajo alipozima moto wao kwa kuwachapa bao la pili baada ya kutengewa pasi safi kwa kichwa na Paul Peter.

Bao hilo lilionekana kuwatoa mchezoni Gwambina kwani dakika ya 90 David Bryson alifunga bao la tatu kwa KMC na kufanya mchezo kumalizika kwa vijana wa Kinondoni kuibuka na ushindi wa bao 3-0.

Ushindi huo umewafanya KMC kupanda mpaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu bara na kuwashusha mabingwa watetezi wa ligi hiyo Simba SC mpaka nafasi ya tano wakiwa weamecheza michezo saba pekee miwili nyuma ya KMC.

KMC  wamefikisha alama 14, baada ya kucheza michezo tisa wakiwa wameshinda mechi nne dhidi ya Gwambina 3-0, Mbeya City 4-0, Tanzania Prison 2-1, Mwadui 2-1, wakipata sare mbili na Coastal Union 0-0 na Ruvu Shooting 1-1, huku wakifungwa mara tatu na Kagera Sugar 1-0, Polisi Tanzania 1-0, Yanga 2-1.

Wenyeji wa mchezo huo Gwambina wao wamesalia kwenye nafasi ya 12, baada ya kucheza mechi tisa na kushinda mbili dhidi ya Ihefu 2-0, na Mtibwa 2-0, wakitoa sare tatu kwa Kagera Sugar 0-0, Polisi Tanzania 1-1, na Coastal Union 1-1, huku wakipoteza mechi nne dhidi ya KMC 3-0, Biashara United 1-0, Simba 3-0, na Ruvu Shooting 1-0.